Na Joyce Kasiki, TimesMajira Online, Dodoma
WADAU mbalimbali wametoa jumla ya sh. milioni 68 kwa ajili ya kumuunga mkono Rais John Magufuli katika mchango aliouanzisha wa ujenzi wa msikiti wa kisasa katika eneo la Chamwino mkoani Dodoma.
Wadau waliotoa fedha hizo ni pamoja na wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama nchini, wakuu wa mikoa na Kanisa la AIC mkoani Simiyu .
Akizungumza kabla ya kukabidhi mchango wa wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama, Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Jenerali Vanance Mabeyo amesema, wameguswa na uamuzi huo wa kutaka kujenga Msikiti bora na wa kisasa katika eneo hilo.
Jenerali, Mabeyo amesema baada ya wazo la Rais Magufuli la kutaka kujenga msikiti huo, aliamua kukaa na wakuu wa vyombo vya ulinzi ambapo walifanikiwa kuchanga kiasi cha sh. milioni 30.
Amesema kiasi hicho cha fedha kilichochangwa imeelekezwa kikabidhiwe kwa mkandarasi wa ujenzi wa msikiti huo ambao ni Jeshi la Kujenga Taifa(JKT) ambapo alikabidhi fedha hizo kwa Meja Jenerali Charles Mbuge kwa utekelezaji,”amesema.
Pia amesema, wakuu wa Idara za vyombo vya ulinzi na usalama nao walihamasika katika jambo hilo na wamechanga kiasi cha sh. milioni 10 ambazo atazikabidhi wakati wowote kuanzia sasa kwa mkandarasi wa ujenzi ambaye ni JKT na kumkabidhi, Meja Jenerali Mbuge.
Naye, Meja Jenerali, Mbuge akipokea fedha hizo aliahidi kazi hiyo kufanyika kwa ukamilifu na kwa wakati huku akiwapongeza wote walijitoa kuchangia na kuunga mkono uamuzi wa rais.
Kwa upande wao wakuu wa mikoa, wamechangia kiasi cha sh. milioni 26 kwa ajili ya kazi hiyo. Akizungumza wakati wa kukabidhi mchango huo, Mkuu wa mkoa wa Pwani, Evarist Ndikilo amesema kuwa kufuatia agizo la Rais, Magufuli, wakuu wa mikoa waliguswa na kuamua kutoa kiasi hicho
cha fedha ili kuwezesha kazi ya ujenzi wa msikiti.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Anthony Mtaka akikabidhi mchango kutoka kanisa la AIC mkoani Simiyu amesema Kanisa limeona ni vyema kuunga mkono juhudi za rais kwa kuchangia fedha hizo.
Naye Sheikhe wa Wilaya ya Chamwino, Suleiman Matitu, akishukuru viongozi hao kwa mchango wao amesema, uongozi wa msikiti Wilaya ya Chamwino, wanamshukuru Rais Magufuli kwa kufanya jambo hilo bila kubagua dini.
Amesema, msikiti huo unatarajiwa kunufaisha kaya zaidi ya 500 zilizopo katika Wilaya hiyo, pia wageni watakaowasili Chamwino Ikulu. “Tunamshukuru sana Rais Magufuli kwa kuwa ndiye mwanzilishi wa jambo na mchakato huu,”amesema.
More Stories
Bodaboda wamchangia Rais Samia Mil 1 ya fomu ya Urais
CCM hakuna kulala, Nchimbi atua Tabora kwa ziara ya siku mbili
Kongamano la Uwekezaji na Biashara lafunguliwa Pwani