Na Daud Magesa,Timesmajira online, Mwanza
BOHARI ya Dawa (MSD) Kanda ya Ziwa imekutana na wadau na wateja wake wakiwemo waganga wakuu,wafamasia na watendaji wa halmashauri kujadili changamoto na kuboresha huduma za afya, upatikanaji wa dawa pamoja na vifaa tiba ili kupunguza kero kwa wananchi.
Kikao kazi hicho cha wadau kinalenga kuunga mkono jitihada za Rais Samia Suluhu Hassan za kuboresho sekta ya afya kwa vitendo kwa kutumia taaluma zao kutoa huduma stahiki kwa wananchi.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara,Msalika Makungu, akizungumza na waandishi wa habari leo Mei 19,2023 jijini Mwanza,amesema,MSD imeamua kurejesha kikao hicho cha wadau ili kukoselewa ,kujenga mazingira ya kupunguza changamoto za pande mbili,kubadilishana uzoefu na kufanya kazi pamoja ya kuwahudumia wananchi wa Tanzania.
Amesema kikao kazi hicho kati ya MSD,wadau na wateja wakiwemo waganga wakuu, wafamasia na watendaji wa Wizara ya Afya na TAMISEMI kwa ajili ya kujadili kuboresha huduma za afya ili kuwezesha bidhaa za dawa na vifaa tiba kupatikana kwa uhakika ili kupunguza kero kwa jamii.
Makungu amemshukuru Rais Dk.Samia Suluhu Hassan kwa uamuzi wa kusimamia na kuwekeza fedha nyingi MSD,uwekezaji ambao ni lazima uakisi mahitaji ya wananchi hivyo watendaji na wadau hao watajadili na kubadilishana uzoefu ili tija ionekane katika uwekezaji huo wa serikali.
“Nawashukuru MSD kuandaa kikao hiki muhimu na kuwakutanisha watendaji wa sekta ya afya kujadili changamoto za mnyororo wa uuzwaji na ugavi wa bidhaa za dawa,nini kifanyike wananchi wapate huduma hizo kwa uhakika na hivyo maboresho yaliyofanywa na Bohari la Dawa yatumike na kuwezesha wananchi kupata huduma zenye tija,”amesema Makungu.
Makungu amesema kupatikana kwa bidhaa za afya MSD kwa sasa hali ni nzuri baada ya kufanyika maboresho mbalimbali,muda wa kusubiri bidhaa ni mdogo na imetoa unafuu kwa kuwatumia wasambazaji wa kati (Prime Vendors),imeingia mikataba na makampuni ya kutoa huduma ili kupata bidhaa bora na kwa wakati.
“Changamoto iliyopo sasa ni makadirio madogo ya bidhaa kwenye vituo wakati mahitaji ni makubwa,hivyo wakadiriaji wajengewe uwezo wakadirie kwa umakini ili kutatua changamoto hiyo,”ameshauri Katibu Tawala huyo wa Mkoa wa Mara.
Pia ili kupunguza vifo vinavyotokana na uzazi pingamizi amesema afya ni mtaji,mtu akiwa na afya bora utendaji na uzalishaji utakuwa mzuri na kuwataka watalaamu kila mmoja kwa nafasi yake atimize majukumu yake kwa weledi ili huduma za afya zinazotolewa ziwafikie wananchi kwa ubora unaotakiwa.
Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mara,Dkt.Zabron Masatu amesema,maelekezo ya Katibu Tawala wameyapokea na wamejipanga kuboresha zaidi huduma hasa upatikanaji wa bidhaa za dawa zifikie asilimia 100 na kuwasimamia watendaji kuhakikisha huduma bora zinapatikana.
“Serikali tayari imewekeza fedha MSD, kazi yetu ni kuhakikisha bidhaa zinasimamiwa kwa usahihi kwenye vituo na zinawafikia wananchi,pia kutumia ubunifu kutatua changamoto wananchi wasikose dawa,”amesema na kuishukuru MSD kuandaa kikao kazi hicho ili wawe na uwezo.
Dkt.Masatu amesema MSD ihakikishe vifaa tiba na dawa wanazoagiza kwa makadirio sahihi zipatikane kwa asilimia 100 pia zipo changamoto zinazoweza kutatuliwa kwa pamoja ikiwemo eneo la maoteo,bajeti za vituo na mahitaji ya bidhaa kulingana na wakati ili kupunguza dawa zinazoteketezwa na kuisababishia serikali hasara.
Naye Meneja wa MSD Kanda ya Ziwa,Egidius Rwezaura amesema ili kukidhi mahitaji ya wadau wameingia mikataba kuhakikisha bidhaa zinapatikana kwa wakati na kuwafikia wadau kwa kiwango kinachohitajika.
“Tumekutana na kukaa na wadau kujadili kwa pamoja changamoto za bidhaa za tiba ya afya kuhakikisha zinapatikana, mipango yetu ni kuboresha huduma za kupata bidhaa hizo ambapo tumeingia mikataba na Central level, bidhaa ziingie na kupatikana kwa wakati tofauti na zamani mikataba ilikuwa ya wakati mmoja,”amesema.
Rwezaura ameeleza ili kukidhi mahitaji ya vituo vya afya na hospitali wamejipanga mwaka wa fedha ujao Julai/Agosti watapokea bidhaa nyingi zinazohitajika vikiwemo vitanda na mashine mbalimbali,wamejiongeza na kuvinunua pamoja na kuvihifadhi.
Aidha Mfamasia wa Halmashauri ya Mji wa Bunda, Teddy Amos,amesema walikuwa na changamoto nyingi za ukosefu wa bidhaa muhimu za dawa walizokuwa wakiomba zilikuwa hazikidhi mahitaji ya wateja,hivyo kikao kazi hicho kitasaidia sana kutatua changamoto hizo.
More Stories
DC Korogwe awataka viongozi wa vijiji kuwatumikia wananchi kwa uadilifu
Premier Bet yamtangaza mshindi mkubwa
Dkt. Kazungu atembelea miradi ya umeme Dar es Salaam