November 6, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wadau waaswa kuwafikia wananchi wanaoishi Pembezoni

Na Mwandishi wetu, TimesmajiraOnline,Mbeya

WADAU wanaotekeleza miradi mbalimbali katika Halmashauri ya Wilaya ya Chunya mkoani Mbeya wametakiwa kupanua wigo wa shughuli zao kwa kuwafikia wananchi wanaoishi maeneo ya pembezoni ili kukabiliana na changamoto za kijamii zinazowakabili, hususan katika malezi na makuzi ya watoto.

Wito huo umetolewa Novemba 5, 2026, na Afisa Tawala wa Halmashauri ya Wilaya ya Chunya, Semwano Mlawa, aliyemwakilisha Mkuu wa Wilaya hiyo katika mkutano wa mwaka wa wadau wa mashirika yasiyo ya kiserikali (NGOs) yanayotekeleza miradi mbalimbali wilayani humo.

Amesema mashirika hayo yanapaswa kuhakikisha yanafika katika maeneo mbalimbali ya wilaya hiyo, ikiwemo maeneo ya pembezoni, badala ya kujikita zaidi katika maeneo ya mjini ambako baadhi ya huduma na elimu tayari zinapatikana kwa urahisi.

“Ni muhimu kufika hata katika maeneo kama Ifumbo na maeneo mengine ya pembezoni ili kuwapatia wananchi elimu na kusaidia kutatua changamoto mbalimbali za kijamii zinazowakabili,” amesema Semwano.

Aidha, ameyahimiza mashirika hayo kuendelea kuandika na kuwasilisha maandiko ya miradi ili kupata fedha zitakazowezesha kuendesha taasisi zao na kutekeleza shughuli za kuwahudumia wananchi katika sekta mbalimbali.

Amesisitiza pia umuhimu wa mashirika kuweka wazi bajeti zinazotumika katika utekelezaji wa miradi na shughuli zao ili kuimarisha uwazi, uwajibikaji na ushirikiano kati ya serikali na jamii.

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Chunya, Janeth Mwaigoga, ameyataka mashirika yasiyo ya kiserikali kuimarisha ushirikiano katika utekelezaji wa shughuli zao ili kuongeza ufanisi na kuhakikisha huduma zinawafikia wananchi wengi zaidi.

Ameahidi kuwa Halmashauri itayashirikisha mashirika hayo katika vikao vya maandalizi ya bajeti ya mwaka wa fedha 2027/2028 ili kutoa maoni na mapendekezo yatakayosaidia kupanga vipaumbele na mgawanyo wa rasilimali kwa kuzingatia mahitaji ya wananchi.

Amesema hatua hiyo itasaidia kuepusha mkusanyiko wa huduma katika eneo moja na badala yake kuhakikisha maeneo mbalimbali yanapata huduma kulingana na mahitaji yake.

Akisoma taarifa ya utekelezaji wa shughuli za mashirika yasiyo ya kiserikali, Zairi Hamisi amesema mashirika hayo yataendelea kuwasilisha taarifa za utekelezaji wa shughuli zao kwa Halmashauri kila robo mwaka.

Ameeleza kuwa pia yataendelea kuzingatia miongozo, taratibu na sheria zinazoyasimamia, ikiwemo kulipa ada ya usajili ya kila mwaka na kuwashirikisha maafisa wa serikali katika ngazi za kata na wilaya wakati wa kutekeleza miradi yao.

Katika mkutano huo, baadhi ya wadau waliwasilisha taarifa za utekelezaji wa miradi mbalimbali kwa mwaka wa fedha 2025/2026, ikiwemo miradi ya maji, ardhi, kuimarisha mifumo ya imani, malezi, makuzi na maendeleo ya mtoto pamoja na miradi ya kubaini na kutatua changamoto za kijamii.

Mkutano huo ulihudhuriwa na wataalamu kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Chunya pamoja na wawakilishi wa mashirika yasiyo ya kiserikali yanayotekeleza miradi wilayani humo, yakiwemo MIICO, CRS, HIMSO, SHAROM na Phidea.

Lengo la mkutano huo ni kuimarisha ushirikiano kati ya serikali na mashirika hayo, kutathmini utekelezaji wa miradi na kujadili changamoto zinazojitokeza katika kuwahudumia wananchi.