January 22, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wadau waaswa kutohofia soko la mkonge

Na Joyce Kasiki,Timesmajira

MKONGE  ni zao ambalo soko lake halitegemei msimu kulinganisha na mazao mengine ambapo mkulima au mfanyabiashara anaweza kuvuna na kuuza wakati wowote katika mwaka.

Akizungumza kwenye Maonesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa (Sabasaba) yanayofanyika Dar es Salaam Afisa kilimo wa Bodi ya Mkonge Tanzania  (TSB),Emmanuel Lutego amesema kutokana na hali hiyo, wadau wanaotaka kuingia kwenye sekta ya Mkonge hawatakiwi kuhofia masoko kwamba watauza wapi au wakati gani kwani moja ya jukumu la Bodi ya Mkonge ni kuwaunganisha wakulima na masoko ya mkonge.

“Kama nchi tuna mkakati wa kufikisha tani 120,000 ifikapo 2025 kwa hiyo tunahitaji wakulima zaidi na mashine za uchakataji ili kufikia malengo hayo”.

Lutego amesema mahitaji ya mkonge duniani ni tani 500,000 lakini zinazozalishwa kwa sasa ni 250,000 huku Tanzania ambayo ni ya kwanza kwa kuzalisha mkonge wenye ubora ikizalisha tani 56,000.

Aidha, ametaja mikakati ya kufanikisha malengo hayo ni kuongeza ukubwa wa mashamba na idadi ya wakulima wa mkonge kwa kuhamisisha na kutoa elimu ya kilimo bora cha mkonge katika mikoa yote inayofaa kwa kilimo cha mkonge.

“Lakini pia tumejipanga kuongeza tija ya uzalishaji, kuongeza uzalishaji wa mbegu bora za mkonge, kuanzisha vituo vya uchakataji wa mkonge(decortication centres) kwa wakulima wadogo,” amesema Lutego.

Amesema wakulima zaidi ya 12,000 wanajihusisha na kilimo hicho nchini ambapo wengi wakiwa ni wakulima wadogo wadogo. 

Amesema vituo vya uchakataji vipo katika Wilaya za Handeni, Mkinga na maeneo mengine ambako mwitikio wa wakulima wa mkonge umekuwa mkubwa.