*Wapinga mapendekezo ya TASHICO ya kutaka meli hiyo kutopita Kemondo ikitoka Mwanza
Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online -Bukoba
Wadau wa usafiri na usafirishaji Mkoa wa Kagera wapinga mapendekezo yaliotolewa na Kampuni ya Meli Tanzania (TASHICO)ya kutaka kufanya safari za meli mpya ya MV.Mwanza kutoka Mwanza kwenda Bandari ya Bukoba bila kupita Kemondo.
Ambapo Mkoa wa Kagera katika sekta ya usafirishaji na biashara kwa kiasi kikubwa unategemea usafiri wa meli kutoka Mwanza hadi Bukoba kupitia bandari za Kemondo.

Hivyo kutokana na umuhimu wa bandari ya Kemondo baadhi ya wadau waliohudhuria kikao cha maoni ya wadau kuhusu mapendekezo ya bei za nauli ya meli mpya ya Mv.Mwanza mkoani humo, wameonesha kutoridhika na mapendekezo hayo.
Ambapo wamesema kuwa yatakuwa na athari kubwa kwa uchumi wa Mkoa na biashara zinazofanyika katika bandari ya Kemondo pamoja na usafirishaji wa mizigo.
Akizungumza katika kikao hicho Ofisa Tarafa Katerero,Bwanku Bwanku, amesema bandari ya Kemondo ni kubwa na ya kisasa yenye uwezo wa kupokea meli kubwa yoyote kutoka duniani na ina jengo la kisasa la abiria.
Bwanku,amesema mapendekezo ya TASHICO ya kufanya safari za Mv. Mwanza kutoka mkoani Mwanza kwenda bandari ya Bukoba bila kupita Kemondo litaleta mgogoro kati ya wananchi na serikali.
“Serikali imeweka fedha nyingi katika bandari hiyo na viongozi mbalimbali wamekuwa wakiitembelea ikiwemo Mawaziri na Balozi.Tumekuwa tukiwaeleza wananchi kuwa meli mpya ya Mv.Mwanza itapitia bandari ya Kemondo halafu leo turudi tuwaeleze eti haitapita hilo jambo haliwezekani,”amesema Bwanku.
Sanjari na hayo amesema vitu vidogo vidogo kama hivyo ndiyo vinasababisha wananchi kuilaumu serikali wakati lengo lake ni kusogeze huduma karibu huku akihoji kuwa miundombinu ipo je kuna sababu gani ya msingi inayozuia meli mpya kupitia katika bandari ya Kemondo?.
Marco Kingunge mdau wa usafirishaji Mkoa wa Kagera,amesema asilimia kubwa ya uzalishaji na usafirishaji mkoani humo ni kutoka Kemondo je ni sababu gani ya msingi inayofanya meli hiyo isipite katika bandari hiyo.
“Ofisa Uendeshaji wa TASHICO,Prosper Rwelengera,ameleza kuwa sababu kubwa ni muda na gharama za uendeshaji,hakuna sababu ya msingi kwa maana kuwa safari ya meli ni mara moja kwa wiki.Sisi wanakagera tunaomba meli mpya ipite bandari ya Kemondo kwani ina mizigo mingi na mikubwa,”amesema.
Pia amesema kwa mwaka jana Serikali imetoa fedha Kwa ajili ya kufanya maboresho ya kisasa ya miundombinu ya bandari hiyo ikiwemo kujenga gati mpya, kupanua eneo la kupakia na kupakua mizigo, na kuboresha huduma za usalama.Ambapo uboreshaji huo ulilenga kufanya bandari hiyo kuwa na uwezo wa kushughulikia mzigo mkubwa na kuimarisha usafirishaji wa bidhaa kutoka na kwenda Mwanza .
Hivyo, wadau hao wamesisitiza kwamba kufanya safari za meli za Mv.Mwanza bila kupita Kemondo kutapunguza faida za uwekezaji huo na kuathiri biashara zinazofanyika kupitia bandari hiyo.

Kwa upande wao baadhi ya wafanyabiashara mkoani Kagera,wameunga mkono maoni yaliotolewa na wadau wa usafirishaji ya kupinga mapendekezo ya TASHICO.
Ambapo wamesema bandari ya Kemondo ni muhimu kwa usafirishaji wa mizigo mingi ya biashara inayohusisha bidhaa za nafaka ikiwemo mahindi,mbolea na bidhaa za ujenzi.
“Bandari ya Kemondo ndiyo kiunganishi kikuu cha usafirishaji wa bidhaa zote kutoka na kuingia Kagera,hivyo kama meli hiyo itasafiri mpaka bandari ya Bukoba bila kupita Kemondo, itakuwa ni pigo kwa wafanyabiashara na wafanyakazi wa bandari hiyo,” amesema mmoja wa wafanyabiashara wa chakula.
Awali Mkurugenzi wa Udhibiti masuala ya Uchumi wa Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC),Nahson Sigalla kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa shirika hilo,amesema lengo la kikao hicho ni kukusanya maoni ya wadau kuhusu mapendekezo ya nauli Mv.Mwanza ambayo yaliondaliwa na TASHICO na kuwasilishwa kwa shirika hilo ambapo kikoa kama hicho kilifanyika mkoani Mwanza Desemba 15 mwaka.
Ofisa uendeshaji wa TASHICO Prosper Rwelengera, akitoa wasilisho la mapendekezo ya nauli amesema, meli hiyo yenye uwezo wa kubeba abiria 1,200 na tani 400 za mizigo itafaya safari zake kutoka bandari ya Mwanza kwenda Bandari ya Bukoba mara moja kwa wiki.
Rwelengera amesema nauli zilizopendekezwa na TASHICO ni shilingi 30,000 kwa daraja la uchumi na daraja la biashara 45,000 huku vyumba vya kulala kuna madaraja matatu tofauti huku baadhi ya wadau wameombwa nauli zipunguzwe kwenye daraja la uchumi na biashara.
Naye Dwani wa Kata ya Bukoba, Shaaban Rashid ameomba nauli ya daraja la uchumi iwe kati ya sh.25,000 na sh.27,000 badala ya sh. 30,000 pamoja na daraja la biashara iwe sh.40 ,000 badala ya sh. 45,000.

Mkuu wa wilaya ya Misenyi Kanali Msaafu Hamisi Maiga kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Kagera Hajjath Fatma Mwassa,amrsema meli hiyo itachechemua uchumi wa mkoa huo kutokana na fursa zilizopo ikiwemo biashara ya mazao ya kilimo,uvuvi, shughuli za ujasiriamali pamoja na usafiri wa majini.
Anasema meli hiyo itafanya safari za haraka zaidi ikilinganishwa na meli nyingine hivyo itakuwa kichocheo cha usafirishaji wa kimataifa katika ziwa Victoria huku akitoa wito kwa TASHICO kuona uwezekano wa meli hiyo kutoa huduma za usafiri wa abiria nchi jirani kama Kenya na Uganda ili kuchechemua uchumi wa mikoa ya Kanda ya Ziwa ikiwemo Kagera.
i




More Stories
Usajili wa Laini za Simu: Jilinde Dhidi ya Kutumiwa Vibaya kwa Utambulisho Wako
TTCL yaadhimisha siku ya Wanawake kwa kutoa msaada JKCI
Wananchi Dodoma washauri TBA kujenga nyumba za kupangisha watu binafsi