Na Bakari Lulela, TimesMajira Online
WADAU wa kazi za sanaa nchini, wakiwemo wanamuziki, watunzi wa ngojera , na vyombo vya habari, wametakiwa kutumia lugha ya kiswahili kwa ufasaha, kuhakikisha wanafikisha ujumbe mzuri kwa jamii inayosikiliza kazi zao.
Rai hiyo imetolewa na Mtaalamu wa lugha ya kiswahili kutoka Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA), Oni Sigala wakati akiwasilisha mada ya matumizi sahihi ya lugha ya kiswahili katika kazi za sanaa kwenywe “Jukwaa la Sanaa” lililoandaliwa na Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA), katika viwanja vya Nafasi Arts Space jijini Dar es salaam.
Sigala amesema, lugha ya kiswahili ni bidhaa ambayo inatumiwa na wasanii mbambali katika utunzi wa kazi zao, hivyo wanatakiwa kutumia maneno mazuri ya kiswahili kufikisha ujumbe kwa hadhira na sio matusi.
“Asilimia 70 ya wasanii hususani wa muziki wa bongo fleva wanatumia maneno ya matusi kwenye nyimbo zao, kuanzia sasa tukisikia nyimbo haifuati maadili mazuri tutatoa mapendekezo kwa wenzetu Basata wachukue hatua ikiwemo kuzifungia hizo,”amesema Sigala.
Awali akifungua Jukwaa hilo, kaimu katibu mtendaji wa Basata, Matiko Mniko amesema Jukwaa hilo la Sanaa limewashirikisha wadau mbalimbali wa sanaa ikiwemo muziki, ngonjela, ushairi, waandaaji wa kazi za sanaa, ikiwa na lengo la kuwapa fursa wadau hao kujadili kuhusu maadili ya sanaa pamoja na kusikiliza maoni na mapendekezo yao ili kuboresha utendaji kazi pamoja na Basata.
“Hii programu ya ‘Jukwaa la Sanaa’ ina fursa ya kukutana na wadau wa sanaa ikiwemo wasanii, tumeanza hapa Dar es salaam lakini tunampango wa kufika katika ngazi za kanda ili kutoa elimu hii kwa wadau, waweze kuzingatia maadili katika kazi zao ikiwa ni pamoja na matumizi sahihi ya lugha ya kiswahili, pamoja na maadili mengine,” amesema Mniko.
Nae mwakilishi wa Jeshi la Polisi Kinondoni, Dr. Ezekiel Kyogo amewataka wasanii ambao kazi zao zinaibiwa au kusambazwa bila ridhaa yao na kuwanufaisha watu wengine wapeleke malalamiko yao katika kituo cha polisi ili wahusika wachukuliwe hatua za kisheria kwani kufanya hivyo ni kosa la jinai.
Kwa upande wao wadau wa sanaa, wamelipongeza Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) kwa kuanzisha programu ya “Jukwaa la Sanaa” huku wakiliomba liendelee kuwashirikisha katika masuala mbalimbali ikiwemo yale yakikanuni waweze kufanya kazi zao vizuri kwa kuzingatia maadili.
More Stories
GETHSEMANE GROUP KINONDONI yaja na wimbo wa siku yetu kwaajili ya harusi
Startimes yazindua makala ya China, Africa
Mwanasheria wa Katavi aliyetimkia kwenye muziki achaguliwa tuzo za MIEMMA