Na Mwandishi Wetu
WADAU wa Sekta Binafsi nchini (TPSF), wameiomba Serikali kupitia upya sheria iliyoanzisha Shirika la Wakala wa Meli Tanzania (TASAC) ili kuondoa changamoto zinazowakabili wafanyabiashara hapa nchini.
Akizungumza na waandishi wa habari mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam mara baada ya mkutano uliowakutanisha wadau wa sekta binafsi na wawakilishi kutoka Serikalini, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TPSF, Zachy Mbenna, alisema TPSF imewaleta pamoja wadau wa sekta hiyo na umma ili kutoa mapendekezo ya nini kifanyike kuboresha huduma za utoaji mizigo na forodha katika Bandari ya Dar es Salaam.
“Tumekuwa na majadiliano muhimu kati ya wafanyabiashara wanaotoa huduma za mizigo na forodha katika Bandari ya Dar es Salaam, tunashukuru kwa kuwa tumeweza kutengeneza nafasi kwa wadau wetu kukutana na wenzetu wa Serikali jambo ambalo litasaidia kuondoa baadhi ya changamoto,” alisema Mbenna.
Alisema kumekuwa na mazingira mazuri ya kimawasiliano kati ya TPSF na Serikali katika kushughulikia changamoto za ufanyaji biashara hapa nchini hali inayowaweka wafanyabishara kwenye wakati mzuri wa kutoa huduma kwa watanzania.
“Siku za nyuma hali ilikuwa tofauti na ilivyo sasa, kumekuwa na ushirikiano mkubwa kati ya taasisi ya sekta binafsi na ile ya umma katika masuala yote muhimu yanayohusu biashara na uwekezaji. Tunaamini mkutano huu utazidi kuleta matokeo mazuri kwa kuwa sekta binafsi ni uti wa mgongo katika kusogeza maendeleo ya Taifa husika,’’ alisema.
Kwa upande wake Katibu Mtendaji Wakala wa Meli Tanzania (TASAA), Abel Uronu, alisema mabadiliko katika uendeshaji wa TASAC ni muhimu kufanyika ili kukidhi haja ya Watanzania kwa kuzingatia gharama, wepesi na utaalamu wa kufanya biashara ndani ya nchi.
“TASAC inadhibiti na pia inafanya kazi ya uwakala kwa wakati mmoja, tunaiomba Serikali iweze kuanngalia sheria iliyoanzishi TASAC mwaka 2017 ili kurahisisha utoaji wa huduma na kuondoa hatari ya kuwa na mgongano wa kimaslahi,” alisema Uronu.
Naye Rais wa Chama cha Usafirishaji wa Mizigo nchini (TAFFA), Edward Urio, alisema kuwa iwapo Serikali itashindwa kufanya mapitio upya ya sheria iliyoanzisha TASAC, itapelekea kukosa kodi kwa kuwa kampuni zaidi ya 800 zitashindwa kujiendesha na hatimaye kufungwa.
“Tunaamini Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais, Dkt. John Pombe Magufuli itasikiliza maoni yetu na kufanyiwa marekebisho ya sheria hiyo ili kuendelea kuzalisha ajira kupitia kampuni zaidi ya 800 zinazojihusisha na uwakala wa meli na forodha na pia upatikanaji wa kodi ambayo itasaidia uendeshaji wa serikali,’’ alisema.
Yosepha Tamam ambaye alikuwa mwakilishi wa timu kutoka Wizara ya Fedha alisema changamoto na mapendekezo yaliyotolewa katika mkutano huo zitafikishwa Serikalini kuangalia namna nzuri ya kuwafanya ili mazingira ya ufanyaji wa biashara hiyo yawe rafiki kwa kila mdau.
TPSF imeahidi kuendelea kuwaunganisha wadau wake wa sekta binafsi na Umma ili kutengeneza mapendekezo ya pamoja ambayo yatachangia kufikiwa kwa haraka azma ya serikali ya kujenga uchumi wa viwanda ifikapo 2025.
More Stories
Mpango ashiriki mazishi ya Mama yake Serukamba
27 kulipwa kifuta jasho Nkasi
Mwakilishi Mkazi wa UN nchini awasilisha hati