Na Mwandishi wetu, Timesmajira
Jukwaa la Tatu la Utekelezaji wa Ushirikishwaji wa Watanzania katika Sekta ya Madini litafanyika Mei 22 hadi 24, 2024 katika ukumbi wa mikutano wa kimataifa wa Arusha International Conference Centre (AICC).
Jukwaa hilo linafanyika kila mwaka limeandaliwa na Serikali kupitia Tume ya Madini chini ya Wizara ya Madini lina lengo la kukutanisha wadau mbalimbali katika Sekta ya Madini kujadili na kufanya tathmini ya ushirikishwaji wa watanzania katika mnyororo wa sekta hiyo.
Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika uzinduzi wa Jukwaa hilo Mei 22, 2024.
Jukwaa hilo lenye kauli mbiu ya “Uwekezaji wa Viwanda vya Uzalishaji wa Bidhaa za Migodini kwa Maendeleo Endelevu,” linaambatana na maonesho ya kampuni mbalimbali zinazojihusisha na shughuli za uchimbaji wa madini nchini, watoa huduma kwenye kampuni za madini na taasisi za kifedha.
Akizungumza leo Mei 17, 2024 Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Mhandisi Yahya Samamba amesema kuwa jukwaa hilo ni utekelezaji wa kanuni za ushirikishwaji wa watanzania katika sekta ya madini na kwamba serikali imeweka mikakati mbalimbali ya kunadi fursa zilizopo katika migodi ya madini.
“Wadau wataweza kupata elimu ya kuwekeza kwenye teknolojia ya kisasa hasa kwenye uendeshaji wa mitambo kuanzia kwenye utafiti, uchimbaji na uchenjuaji wa madini kwa kubadilishana uzoefu na maarifa,” amesema Mhandisi Samamba.
Pia amesema kuwa, lengo la Tume ya Madini ni kuhakikisha inasambaza elimu kuhusu fursa zilizopo katika Sekta ya Madini kwa wadau wa madini nchini katika sekta zote watakaoweza kujiajiri kupitia utoaji wa huduma muhimu kwenye migodi kama vile utoaji wa ushauri wa kifedha, vyakula, ulinzi na kujipatia kipato huku serikali ikikusanya mapato yake yanayotokana na kodi mbalimbali.
Amesema, ongezeko la ushiriki wa watanzania katika sekta ya madini litachangia kukua kwa Pato la Taifa kupitia sekta hiyo.
More Stories
Mhandisi Samamba awasisitiza maafisa madini kusimamia usalama wa migoni msimu wa mvua
Wapinzani kutimkia CCM ishara ya ushindi Uchaguzi Serikali za Mitaa
Vikundi Ileje vyakabidhiwa mikopo ya asilimia 10, DC Mgomi avipa somo