November 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wadau sekta ya habari, waomba vifungu vya sheria kurekebishwa

Na Penina Malundo, Timesmajira Online

WADAU wa sekta ya habari wameitaka serikali kurekebisha vifungu ambavyo havijafanyiwa marekebisho katika Sheria ya Huduma ya Vyombo vya Habari ya mwaka 2016 kulingana na uamuzi wa Mahakama ya Afrika Mashariki (EACJ) ili kuboresha mazingira bora ya vyombo vya habari nchini.

Ripoti zinaonyesha kuwa mwaka 2019, EACJ ilitoa hukumu iliyokiuka vifungu 16 vya Sheria ya Huduma za Vyombo vya Habari ya mwaka 2016 kinyume na kanuni za msingi na za kiutendaji za Jumuiya ya Afrika Mashariki zilizoainishwa katika Ibara ya 6(d) na 7(2) ya Mkataba huo.

Akizungumza katika warsha iliyoandaliwa na Taasisi ya Zaina Foundation kwa Waandisi wa habari,Mawakili pamoja na watu wa Taasisi mbalimbali,Mshauri wa Sera kutoka Taasisi ya Zaina , William Kahale alisema katika maboresho ambayo waliomba kama wadau wa habari kupitia mahakama hiyo ni maboresho matano ndio yamefanyiwa kazi.

Amesema bado kuna umuhimu ya kuboresha vifungu vilivyobaki ili kuzidi kuboresha mazingira ya waandishi wa habari na ufanyaji wa kazi katika sekta ya habari.

”Warsha hii ilikuwa na umuhimu na kukumbusha serikali pamoja na wadau mbalimbali wanaohusika kuweza kuzingatia mabadiliko mengine ambayo hayakutiliwa maanani katika maboresho ya mwaka jana,ambapo yakifanyika yataongeza uwanda wa upatikanaji wa habari na ufanyaji kazi mzuri kwa vyombo vya habari”amesema.

Akitaja miongoni mwa vipengele wanavyotaka vifanyiwe marekebisho ni pamoja na Kifungu cha 19 cha Sheria ya Huduma ya Vyombo vya Habari ya mwaka 2016 kuhusu ithibati ya wanahabari, ambapo mtu hawezi kufanya kazi isipokuwa kama ameidhinishwa, na kifungu cha 20 kinachotaka waandishi wa habari kupewa kadi ya mawasiliano baada ya kupata ithibati.

Zaidi ya hayo, amesema Kifungu cha 36 kuhusu mabadiliko ya vyombo vya habari, Kifungu cha 37 kuhusu ufafanuzi wa uchapishaji usio halali, na Kifungu cha 39 kuhusu kesi ambazo uchapishaji unaruhusiwa kwa masharti, miongoni mwa mengine.

Amevitaja baadhi ya vifungu vilivyofanyiwa marekebisho kuwa ni pamoja na kufuta kashfa maana yake kesi za kashfa zitasikilizwa chini ya mashauri ya madai badala ya jinai; kupunguza adhabu kwa kukiuka vifungu mbalimbali vya sheria, vinavyohusu faini na vifungo vya jela; na kuondoa mamlaka ya Mkurugenzi wa Idara ya Huduma za Habari kuratibu matangazo ya serikali, jambo ambalo litaongeza uwezekano wa vyombo vya habari binafsi kupata matangazo hayo na kuongeza mapato.

Amebainisha kuwa uhuru wa kujieleza unaunga mkono uhuru wa mtu binafsi au jamii kueleza maoni na mawazo yao bila hofu ya kulipizwa kisasi, kuhakikiwa au kuwekewa vikwazo vya kisheria.

Kutokana na hali hiyo, amesema wakati nafasi ya uhuru wa vyombo vya habari imeboreka, fahirisi ya Tanzania World Freedom Press index bado iko chini kwa sababu sheria hazijabadilika.

Akitaja kuwa mwaka 2023 Tanzania ilishika nafasi ya 143/180, juu kidogo ya nafasi ya 2022 ya 123/180,.

Kwa upande wake Mjumbe wa Bodi ya Taasisi ya Zaina,Ibrahim Samata amesema kuwa ipo haja ya kuangalia vipengele vya Sheria ya Huduma ya Vyombo vya Habari ya mwaka 2016 vinavyokiuka uhuru wa kujieleza.

Amesema miongoni mwa sehemu zinazokiuka uhuru wa kujieleza ni pamoja na ithibati ya wanahabari, ambayo inawataka wanahabari wote wanaofanya mazoezi kuwa na kadi.

Amebainisha kuwa kuna utofauti kati ya waandishi wa habari, lakini kadi za vyombo vya habari huwekwa kati na kutolewa sehemu moja, hivyo kuhitaji ziwekwe kwenye mfumo wa kidigitali ili kuwawezesha waandishi wa habari popote pale nchini kuweza kuzipata mara moja.

“Pia kuna suala la madaraka ya mawaziri kuweza kukuza uhuru wa vyombo vya habari; tuwe na chombo huru badala ya kumtegemea waziri kufanya maamuzi kwa kila jambo,” amesema Samata.