September 29, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wadau Korogwe wataka falsafa ya 4R itumike uchaguzi Serikali za mitaa

Na Yusuph Mussa,Timesmajiraonline,Korogwe

BAADHI ya wadau katika Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe mkoani Tanga wamesema ili Uchaguzi wa Serikali za Mitaa ufanyike kwa amani, utulivu na kuaminiana inabidi itumike falsafa ya R4 za Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan.

Wamesema R4 za Rais Dkt. Samia zitaondoa ‘makovu’ kwa baadhi ya vyama vya siasa kutokana na malalamiko ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa wa mwaka 2019, ambapo baadhi ya viongozi wa vyama vya siasa wanadai haukufanyika kwa uhuru na haki.

Amesema hayo mwishoni mwa wiki kwenye kikao cha wadau wa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe kilichowashirikisha viongozi wa vyama vya siasa, viongozi wa dini, asasi, watumishi wa halmashauri na Serikali za Mitaa, na kufanyika Ukumbi wa Halmashauri wa zamani.

Katibu wa Umoja wa Wazee Wilaya ya Korogwe Hamis Kaniki alisema kama sheria, kanuni na taratibu zitafuatwa, huku R4 za Rais Dkt.Samia kama zitafuatwa, basi Watanzania watavuka salama kwenye uchaguzi huo.

“Hiyo sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa zikitumika vizuri, mimi nina uhakika tutapita salama. Na wala hakuna sababu ya kuwa na hofu na polisi. Polisi utamuita pale utakapokuwa umemaliza kupiga kura, lakini umeendelea kubaki kwenye kituo, ni sawa na kumualika polisi aweze kufika, hivyo tukifuata sheria, kanuni na taratibu za uchaguzi, tutatoka salama.

Kaniki ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati ya Amani ya Viongozi wa Dini Wilaya ya Korogwe, amesisitiza kuwa pamoja na vyama vya siasa kupata misukosuko kwenye Uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka 2019, bado wanatakiwa kumuunga mkono Rais Dkt. Samia kwa Falsafa yake ya R4 ili kuona nchi inaendelea kuwa na amani, na sio kwenye uchaguzi, bali nyakati zote.

“Lakini Mama yetu, Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ametuletea Four R (4R) kama nyongeza… Reconciliation (Maridhiano). Mfike hatua mnatofautiana, lakini lazima mtafute maridhiano. Haitoshi hiyo, Mama akatuletea Resilience (Ustahimilivu). Lazima tuvumiliane kwa kutofanya mambo kwa jazba. Tuna Reforms (Mageuzi). Tusiangalie tulikotoka, bali tuangalie tunakokwenda. Jamani hata kama unataka kula bata, lakini ukitaka kuchunguza kitu alichokula bata, hutaweza kumla. Hivyo, kule tulikotoka 2019, changamoto zake zinatatuliwa na 4R.

“Inakuja Rebuilding (Kujenga), tunajenga upya. Yaani yale yaliyotokea tulikotoka na yale yote, tukizingatia four R za Mama (Rais Dkt. Samia) tunatoka salama. Kwa hiyo mimi nitoe rai, na niombe, tuzitumie hizi 4R za Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, tutatoka salama. Tukizitumia hizi, hata maombi ya sisi viongozi wa dini yatapenya. Ndugu zangu wa ACT- Wazalendo, CHADEMA na wengine, najua mlipita kwenye maumivu makali, lakini 4R hizi tuzitumie vizuri” alisema Kaniki.

Naye Mwenyekiti wa ACT Wazalendo Jimbo la Korogwe Vijijini Mussa Majaliwa maarufu kama Kipepe, amelitaka Jeshi la Polisi kuweka uwiano sawa wa kufanya kampeni kati ya vyama vya siasa na chama tawala, Chama Cha Mapinduzi. Na kuongeza kuwa, chama chochote kisitoe mamluki Jimbo la Korogwe Mjini kwenda kugombea nafasi yeyote kwenye uchaguzi huo Jimbo la Korogwe Vijijini.

Katibu wa CCM Wilaya ya Korogwe Vijijini Safina Nchimbi amevitaka vyama vya siasa kuheshimu sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa kwenye Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, kwani uzoefu unaonesha, wao viongozi wa vyama vya siasa ndiyo watu wa kwanza kutaka kuleta vurugu kwenye kampeni, na hata siku ya uchaguzi. Na ili kuondoa mkanganyiko kwa wasimamiaji wa uchaguzi pamoja na polisi, chama cha siasa kikisema watakuwa na mkutano wa kampeni kwenye kata fulani, wataje na kijiji ama kitongoji husika, na sio kuvamia kwenye shughuli za maendeleo, minada ama masoko.

Msimamizi wa Uchaguzi Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe Goodluck Mwangomango ameahidi kuwa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa utatoa haki kwa vyama vyote vya siasa katika ratiba za kufanya kampeni, na stahiki zote zitakazowasaidia viongozi wa vyama vyote kutimiza majukumu yao kwenye uchaguzi huo.