Na Joyce Kasiki,Timesmajira online,Dodoma
HATIMAYE mgogoro wa Kanisa la EAGT uliodumu kwa kipindi cha miaka sita umemalizika na hivyo kuondoa mgawanyiko uliokuwepo katika Kanisa kutokana na mgogoro huo huku wachungaji walioliasi Kanisa hilo wakipewa wa kuomba msamaha ili warejee kufanya kazi ya Mungu kanisani humo.
Akizungumza na waandishi wa Habari katika Makao Makuu ya Kanisa hilo jijini Dodoma,Askofu Mkuu wa Kanisa hilo Brown Mwakipesile amesema,mgogoro huo umemalizika baada ya maamuzi ya uongozi wa Msajili wa Jumuiya ya Kanisa hilo kutoa barua yenye kumbukumbu Na.SA. 7183/PARTVI/50 ya 30 Juni 2022.
Amesema,barua hiyo ina maelezo ya kina jinsi Serikali ilivyofanya Uchunguzi wa kutosha na mwishowe ikabaini kwamba tuhuma zote walizotuhumiwa Viongozi Wakuu wa Kanisa la EAGT hazina msingi na wala Viongozi hao Wakuu hawahusiki kabisa na tuhuma zote walizotuhumiwa nazo.
“Jambo ambalo limeipa ujasiri Serikali yetu kutangaza kwamba, mgogoro umekwisha na kutambua Viongozi halali wa Kanisa la EAGT kwa sasa kwa kuorodhesha majina yao jambo ambalo limefuta kabisa mawazo potofu yaliyokuwa yanaenezwa kwamba kuna EAGT mbili.”amesema Askofu Mwakipesile
Kufuatia hatua hiyo , ametaja viongozi halali wa Kanisa hilo kuwa ni Askofu Mkuu Dkt. Brown Mwakipesile, Makamu Askofu Mkuu Dkt. Joshua Wawa,Katibu Mkuu Dkt. Leonard Mwizarubi,Muhazini Mkuu Dkt. Praygod Mgonja na Mshauri Mkuu Dkt. Livingstone Dennes
“Mgogoro wa Kanisa ulitokana na aliyekuwa Makamu Askofu Mkuu wa kanisa letu John Stephene Mahene kupinga kuondolewa madarakani kwa sababu za kukiuka miongozo ya imani ya kanisa letu ambapo alidai kuondolewa kwa sababu za kuhoji ubadhilifu wa fedha na mali za kanisa uliofanywa na viongozi wa kanisa.”alieleza chanzo cha mgogoro huo
Askofu Mwakipesile amesema,kutokana na kumalizika kwa mgogo huo Kikao cha Baraza la Waangalizi wa Kanisa la EAGT kilichoketi Julai 12 mwaka huu kimetoa miezi mitatu kwa Mchungaji yeyote atakayetaka kurejea baada ya mgogoro kumalizika, kwa kuandika barua ya kutambua kosa lake ndipo aweze kupokelewa.“Mchungaji yeyote atakayetaka kurejea baada ya mgogoro kumalizika,atapokelewa na ngazi husika kwa sharti la kuandika barua kwa Uongozi husika kwamba ametambua kosa lake na sasa anaomba msamaha na kwamba yuko tayari kutumika chini ya Uongozi halali wa Kanisa la EAGT.”amesema
Amfafanua kuwa mwisho wa kupokelewa ni 20 Octoba 2022 na mlango wa maombi hayo ya msamaha utakuwa umefungwa.
Aidha amesema kwa wale ambao watataka kuondoka EAGT, Baraza la Waangalizi limewataka waheshimu Katiba ya EAGT Toleo la 2011 Ibara ya IX ambayo inasema,”Mtumishi aachapo utumishi wake EAGT ataondoka pekee pasipo washirika wala mali za Kanisa”.
Ametumia nafasi hiyo kuwasihi watanzania wotekushiriki katika zoezi la Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022 inayotarajiwa kufanyika 23 Agosti, 2022 ikiwa ni zoezi muhimu kwa kila mtu kuhesabiwa ili kuiwezesha Serikali kuendelea kuweka mipango mbalimbali ya kimaendeelo kwa kujua idadi ya watu wake.
More Stories
CCM imejipanga kushinda kwa kishindo
Wanaotumia lugha za matusi,kashfa kwenye kampeni waonywa
Polisi Mbeya yawataka waandishi wa habari kutoa taarifa sahihi