December 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wachimbaji wanawake waililia serikali ukopeshwaji mitaji

Judith Ferdinand,TimesMajira Online,Mwanza

Imeelezwa kuwa mitaji,vitalu na vitendea kazi ni miongoni mwa changamoto zinazowakabili wanawake katika sekta ya madini nchini,hivyo ombi limetolewa kwa serikali kuungana na taasisi za kifedha ili wanawake hao waweze kukopeshwa mitaji.

Akizungumza na Timesmajira online katika maonesho ya madini yaliyofanyika katika uwanja wa Rock City Mall jijini Mwanza,Mwenyekiti wa Wachimbaji Wanawake Mkoa wa Geita(Gewoma), tawi la Tawoma Asia Masimba,ameeleza kuwa changamoto hizo ndio kilio chao cha siku zote kwa serikali nchini.

Mwenyekiti wa Wachimbaji Wanawake Mkoa wa Geita(Gewoma), tawi la Tawoma Asia Masimba,

Hivyo wanaiomba serikali kuwasaidia mitaji kupitia mikopo ya benki na leseni zao zitumike kama dhamana kwa ajili ya uchimbaji wa madini kwani wana uhakika watarejesha fedha za mikopo.

“Wachimbaji wanawake hatukopesheki, tunapewa mizunguko mingi ambayo haina mashiko,tunaiomba serikali itusaidie kwenye hili mwanamke siyo mzurumati,ana malengo na mipango katika maisha yake ya kuangalia familia yake na analipa kodi kama serikali inavyotaka,”.

Ameeleza kuwa changamoto nyingine ni ukosefu wa vitalu vya uchimbaji wa madini lakini kupitia maonesho hayo wamemsikia Mkuu wa Mkoa wa Geita Martine Shigela akiwatamkia neno zuri mbele ya Waziri Mkuu kwamba watawaga vitalu kwa ajili ya uchimbaji wa madini na wanawake ndio watakuwa kipaumbele.

“Wasiishie tu kutupa vitalu waje watuwekee watu wa kupima waangalie kiwango cha madini yaliopo pale ili tuweze kukopesheka kwenye benki,tukikopeshwa miaka inayokuja 2024/25 tutakuwa wanawake shupavu,imara na wenye fedha,” amesema Masimba.

Sanajari na hayo ameeleza kuwa wakiwawezesha mitaji,vitendea kazi pamoja na vitalu serikali itajivunia wanawake kuwa na fedha kwa sababu siyo wachoyo ni walezi,mawazo mgando yamepitwa na wakati na kwa sasa wanawake wapo imara na wanafanya kazi kwa bidii na weledi zaidi katika sekta ya madini.

Kwa upande wake Katibu wa Kikundi cha wanawake wachimbaji Nyanghwale tawi la Tawoma Geita Veronica Makonge, ameeleza kuwa kwa sasa wanawake nao wanataka wachimbe hivyo ombi lake kwa serikali ni ni kuwawezesha mitaji kwani walionayo ni midogo.

“Tunapopewa maeneo ya uchimbaji madini na seriakali tunaiomba Stamico waingilie kati kutupimia,ili tunapowekeza kile kidogo tulichonacho tuweze kunufaika maana tunapofanya uchimbaji holela wa kuchimba hapa mara pale na haupati kitu kumbe umeacha mwamba sehemu nyingine,”ameeleza.

Katibu wa Kikundi cha wanawake wachimbaji Nyanghwale tawi la Tawoma Geita Veronica Makonge

Pia ameiomba serikali kuwekeza mitaji kwa wanawake kwani ndio wanao tunza familia ili waweze kuendesha miradi yao ya uchimbaji wa madini vizuri na kuwa na nguvu kama wanaume walivyoonekana tangu awali kuwa ndio wenye nguvu katika sekta ya madini.

Aidha ameeleza kuwa wanawake asilimia kubwa wamejichanganya migodini na wanafanya kazi kama zilivyo sekta nyingine na kupangilia muda wa kuhudumia familia pamoja na kufanya kazi hiyo.

Hata hivyo Naibu Waziri wa Madini Dkt. Steven Kiruswa, akizungumza katika kilele cha wiki ya maonesho ya madini liliofanyika katika jijini Mwanza ameeleza kuwa Wizara kupitia Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) linaendelea kuwaunganisha wachimbaji wadogo na taasisi za fedha.

Rais wa FEMATA John Bina, ameeleza kuwa FEMATA imedhamiria kwenda pamoja na wanawake ambapo mpaka sasa takwimu zinaonesha kwamba zaidi ya wanawake 2000 wamejiunga katika shughuli za madini ikiwemo uchimbaji, uchenjuaji na uongezaji thamani madini.

Aidha Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Adam Malima amesema mkoa huo umedhamiria kuwapa leseni wachimbaji wadogo wa madini huku wachimbaji wadogo wanawake wamepewa kipaumbele katika kupatiwa maeneo ya uchimbaji madini.