January 10, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wabunifu Vipimo,Teknolojia mpya wahamasishwa kuchangamkia fursa

Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online

MENEJA wa Viwango na Uhakiki, Wakala wa Vipimo Tanzania (WMA), Magesa Biyani ametoa rai kwa wabunifu wa vipimo pamoja na teknolojia mbalimbali zinazohusiana na uhakiki wa vipimo kuchangamkia fursa kwani sekta hiyo inakua kwa kasi jambo linalokwenda sambamba na uhitaji wa vipimo vya kisasa na teknolojia mpya za uhakiki wake.

Biyani, Ameyasema hayo wakati akiwasilisha mada kuhusu majukumu ya WMA kwa Wakufunzi wa Chuo cha Teknolojia Dar es Salaam (DIT), Agosti 20, 2024.

Meneja wa Viwango na Uhakiki, Wakala wa Vipimo Tanzania (WMA), Magesa Biyani, akiwasilisha Mada kuhusu majukumu ya WMA kwa Wakufunzi wa Chuo cha Teknolojia Dar es Salaam (DIT), Agosti 20, 2024. Biyani ametoa rai kwa wabunifu wa vipimo pamoja na teknolojia mbalimbali zinazohusiana na uhakiki wa vipimo kuchangamkia fursa kwani sekta hiyo inakua kwa kasi jambo linalokwenda sambamba na uhitaji wa vipimo vya kisasa na teknolojia mpya za uhakiki wake.

Akidadavua kuhusu uhakiki wa vipimo ambao ni jukumu la msingi la WMA, Biyani amesema Wakala hiyo inaendelea kuongeza wigo wa utendaji kazi wake kwa kuzifikia sekta mbalimbali ambazo zinachangia kwa kiasi kikubwa katika uchumi wa nchi.

Ametolea mfano wa baadhi ya sekta hizo kuwa ni pamoja na umeme, gesi asilia, mafuta, maji, mawasiliano, usafiri na nyingine nyingi na kufafanua kuwa tayari wamekwishaanza utekelezaji kwa baadhi yake, kazi ambayo ni endelevu yenye malengo ya kuzifikia sekta zote zinazojihusisha na vipimo.

“Kutokana na kukua kwa kasi kwa sekta ya vipimo, natoa rai kwa wasomi na wabunifu mbalimbali kubuni vipimo vya kisasa pamoja na teknolojia mpya na rafiki kwa mazingira ya nchi yetu kwa ajili ya uhakiki wa vipimo,” amesisitiza.

Biyani amempongeza mmoja wa Wahadhiri wa DIT, Georgia Rugumira anayeendelea na zoezi la kubuni Mzani utakaotumika kupima bidhaa mbalimbali.

Hata hivyo, amemkaribisha kutembelea Wakala wa Vipimo ilia pate mwongozo na ushauri zaidi kwa ajili ya kufanikisha ubunifu wake.

Aidha, amewakaribisha na kuwahamasisha Wahadhiri na wanafunzi wa Chuo hicho kutembelea WMA ili kubadilishana uzoefu na kujifunza kwa vitendo kwa ajili ya kupata wataalamu wabobevu katika sekta ya vipimo watakaotoa mchango mkubwa katika kukuza uchumi wa nchi na wa mwananchi mmoja mmoja.

Kwa upande wake, Mkuu wa Idara ya Uhusiano wa Viwanda na Mwongozo wa Kazi kutoka DIT, Dkt. Sosthenes Karugaba ameishukuru WMA kwa kuona umuhimu na kutenga muda wa kuwapatia wakufunzi wa chuo hicho elimu kuhusu vipimo sahihi.

“Kwa niaba ya wakufunzi wenzangu, ninatoa shukurani za dhati kwa WMA juu ya ugeni wenu hapa. Tumejifunza mengi kuhusu vipimo na tumepata maarifa katika maeneo mbalimbali ya kiufundi.

“Tutaandaa utaratibu rasmi wa kuja kuwatembelea huko WMA ili kujifunza zaidi. Tutakuwa mabalozi wazuri wa matumizi sahihi ya vipimo katika jamii,” amesema.

Awali, akiwasilisha Mada kwa Wahadhiri hao wa DIT, Afisa Vipimo kutoka WMA, Jadi Kijumu alibainisha kuwa Wakala hiyo iliyoanzishwa mwaka 2002, iko chini ya Wizara ya Viwanda na Biashara ikiwa na jukumu kuu la kumlinda mlaji wa bidhaa na huduma kupitia matumizi sahihi ya vipimo.

Kwa upande mwingine, alisema WMA humlinda muuzaji wa bidhaa na huduma kwa kuhakikisha anapata faida stahiki kulingana na mauzo ya bidhaa na huduma anayotoa.

Wakala wa Vipimo imejiwekea utaratibu wa kutoa elimu sahihi ya matumizi ya vipimo na kuwapa ushauri wa kitaalamu wadau mbalimbali ili kuwajengea ufahamu na kutatua changamoto mbalimbali za masuala ya vipimo.