December 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wabunge kuelimishwa kuhusu PURA, wiki ya Nishati

Na Penina Malundo,TimesMajira,Online

WABUNGE  na viongozi mbalimbali wa Serikali wanatarajiwa kuelimishwa kuhusu Mamlaka ya Udhibiti Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA) na shughuli inazozitekeleza kwenye Maonesho ya Majukumu ya Wizara ya Nishati na taasisi zake.

Maonesho hayo yaliyoanza rasmi juzi  katika viwanja vya Bunge jijini Dodoma yanaongozwa na kaulimbiu isemayo ‘Nishati kwa Maendeleo Endelevu’ na yatafikia tamati Mei 26, 2022.

Kwa mujibu wa Waziri wa Nishati  January Makamba, amesema  maonesho hayo yanalenga kujibu maswali ya wabunge juu ya masuala mbalimbali ya sekta ya nishati na kutatua changamoto mbalimbali zinazohusiana na sekta.

Amesema wataalamu wa PURA wamejipanga kuongeza uelewa kwa wabunge hao kwa maeneo mbalimbali ikiwemo ya mradi wa kubadili gesi asilia kuwa kimiminika (LNG), ushiriki wa wazawa kwenye miradi mbalimbali ya sekta ndogo ya mafuta na gesi asilia pamoja na fursa mbalimbali zinazopatikana kwenye utekelezaji wa miradi ya mkondo wa juu wa petroli.

Kwa upande wake Mjiolojia kutoka PURA,Ebeneza Mollel amesema kuwa maonesho haya ni jukwaa muhimu kwa PURA kuwafikia wananchi kupitia viongozi wao kwa kuwaongezea uelewa na namna bora ya kutumia fursa zinazopatikana katika utekelezwaji wa miradi mbalimbali ya mafuta na gesi asilia.

“Viongozi hawa ni kundi muhimu kufahamu fursa hizi kwani wanaweza kufikia wananchi kwa urahisi zaidi ikiwa ni pamoja na kuwasaidia na kuwajengea uwezo wa jinsi ya kuchangamkia fursa hizi,” amesema  

Naye Mjiolojia Wangese Matiko kutoka taasisi hiyo ya PURA amesema kuwa wabunge watakaotembelea banda la PURA pia watapata fursa ya kujifunza masuala ya kiufundi kama ya mnyororo wa thamani wa mafuta na gesi asilia, shughuli za utafutaji na uzalishaji zinazoendelea nchini na mengineyo.