Na Joyce Kasiki, TimesMajira Online, Dodoma
TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURUu) imeanza kuwahoji wabunge na waliokuwa wabunge wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kutokana na malalamiko ya baadhi yao kuwa wamekuwa wakikatwa fedha tangu mwaka 2016 lakini hayajulikani matumizi yake.
Wabunge nane walihojiwa jijini Dodoma jana katika ofisi wa TAKUKURU jijini Dodoma ikiwa ni siku ya kwanza ambapo wabunge 69 wanatarajiwa kuhojiwa.
Wabunge waliohojiwa ni Joseph Mbilinyi- Sugu (Mbeya Mjini), Mchungaji Peter Msigwa (Iringa Mjini), Halima Mdee (Kawe), Esther Bulaya (Bunda Mjini) na Ester Matiko).
Wengine wabunge waliotangaza kukihama chama hicho, Peter Lijualikali (Kilombero) na David Silinde (Momba) na Wilfred Lwakatare Mbunge (Bukoba Mjini).
Mbunge aliyekuwa wa kwanza kufika ofisi za TAKUKURU kwa ajili ya kuhojiwa ni Sugu, ambaye alifika saa 1:55 asubuhi na kuhojiwa kwa takribani saa mbili hadi saa 4 asubuhi.
Mbunge wa Kilombero Peter Lijualikali alifika TAKUKURU majira ya saa 2:20 asubuhi, huku Mchungaji Msigwa akifika katika ofisi hizo saa 4:15 asubuhi.
Bulaya na Mdee waliingia pamoja majira ya saa 5:00 asubuhi na kumaliza mahojiano majira ya 7:10 mchana .
“Siku zote mti wenye matunda ndiyo unaopigwa mawe,” amesema Bulaya alipokuwa akitoka kwenye ofisi za TAKUKURU. Kwa upande wa Silinde, aliingia ofisi hizo saa 5:41 asubuhi na kutoka saa 8:31 mchana.
Miongoni mwa wabunge waliozungumza na waandishi mara baada ya kuhojiwa ni pamoja na Lijualikali ambaye amesema; “TAKUKURU imejipanga katika zoezi hilo na linafanywa kirafiki zaidi.”
Alitumia fursa hiyo kuwashauri wahojiwa wote kuwa wakeli, kwani mchakato mzima wa suala la matumizi ya fedha ndani ya CHADEMA walikuwa wanaufahamu.
“Nawaomba ndugu zangu wote ambao wataitwa kuhojiwa kuwa wakweli na kueleza kile wanachokijua maana hawawezi kudanganya chochote kwa namna TAKUKURU wanavyolifahamu hili jambo na wanachokifanya ni kutaka uthibitisho tu,”amesema Lijualikali.
Lijualikali amesema hakuna mwenye nia ya kumsingizia mtu wala kuudanganya umma kwa namna yoyote ile. Kwa upande wake, Silinde aliwataka wahojiwa wote kuzungumza ukweli wa jambo hilo kwani mambo yote yapo bayana.
TAKUKURU imeanza jana kuwahoji wabunge wa CHADEMA na waliowahi kuwa katika chama hicho pamoja na viongozi wa chama hicho kufuatia malalamiko ya baadhi wa wabunge kwamba wamekuwa wakikichangia chama hicho kila mwezi mamilioni ya pesa, lakini fedha hizo hazijulikani matumizi yake.
Jumla ya wabunge 69 wanatarajiwa kuhojiwa na taasisi hiyo na kwa siku ya kwanza tayari wamehojiwa wabunge 8.
More Stories
Waziri Chana amuapisha Kamishna uhifadhi NCAA, ampa maagizo mazito
Amos Lengael Nnko afariki kwa ajali ya gari
Gridi za Tanzania, Kenya kuimarisha upatikanaji wa umeme