October 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Waandishi watakiwa kuandika taarifa sahihi

Na Said Hauni, TimesMajira Online, Lindi

KATIBU Tawala Mkoa wa Lindi, Rehema Madenge amewataka waandishi wa habari kutumia taaluma yao, kuelimisha na kuwapa wananchi taarifa sahihi shughuli zinazofanywa na serikali, ikiwemo utekelezaji unaofanywa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF).

Rehema alitoa wito huo wakati akifungua kikao kazi cha kujenga uelewa kuhusu utekelezaji kipindi cha pili cha awamu ya tatu ya TASAF kwa waandishi wa Mikoa ya Lindi, Pwani, Mtwara na Ruvuma kilichofanyika mjini hapa.

Akifungua kikao hicho kilichojumuisha waandishi 40, amesema waandishi wana majukumu makubwa katika kuelimisha na kuhabarisha umma mambo mbalimbali mazuri na mabaya yanayotokea.

Amesema kuwa, ili Taifa liweze kusonga mbele, waandishi wana nafasi kubwa ya kuwahabarisha wananchi, wakiwemo wa kipato cha chini, kaya zinazoishi katika mazingira magumu ambao ni walengwa wa TASAF, zifanye kazi kwa bidii kwa lengo la kuupiga vita umaskini.

Katibu Tawala huyo amesema, waandishi wanapopata uelewa kuhusu majukumu yanayotekelezwa na TASAF, inakuwa vizuri kwani wananchi watapata taarifa sahihi na ubora unaohitajika, bila ya kuwa na upotoshaji kwa wanaowategemea kuwapatia taarifa husika.

Tangu TASAF ianzishwe miaka 20 iliyopita, miradi mbalimbali imetekelezwa ikiwemo ya elimu, afya, maji, mazingira, ujenzi wa miundombinu ya barabara na masoko.

Pia amesema kuwa, wananchi wa maeneo mbalimbali hupata taarifa za utekelezaji wa miradi husika kupitia vyombo vya habari, hivyo kwa kutambua mchango na faida zake katika kuelimisha wananchi, serikali na taasisi nyingine zikiwemo za umma na binafsi imekuwa mstari wa mbele kuwatumia.

Awali akimkaribisha kufungua kikao kazi hicho Mkurugenzi wa Programu wa TASAF, Amandus Kamagenge amesema, lengo la kikao kazi hicho ni kuwajengea uelewa waandishi wa habari wa mikoa hiyo minne kuhusu utekelezaji wa kipindi cha pili cha awamu ya tatu ya mfuko huo.

Kamagenge amesema, utekelezaji wa awamu hiyo, ulikuwa utekelezwe mapema lakini kuibuka kwa ugonjwa wa Covid-19, ulisababisha kusimamisha kwa shughuli za TASAF licha ya uhakiki wa kuzitambua kaya zinazoishi katika mazingira magumu kukamilika.