March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Waandishi wa habari watakiwa kujikita katika uandishi unaojenga taifa

Na Judith Ferdinand, Timesmajira Online-Dodoma

Waandishi wa habari nchini,wametakiwa kujikita katika uandishi unaochochea umoja,mshikamano na unaolenga kujenga taifa hasa kipindi hiki ambacho jamii na nchi inahitaji utulivu.

Hayo yamezungumzwa Novemba 27,2025, na Mwenyekiti wa Taasisi ya Vyombo vya Habari Kusini mwa Afrika – Tawi la Tanzania (MISA Tanzania), Edwin Soko,katika mafunzo ya siku moja ya uandishi wa habari za amani yaliofanyika jijini Dodoma.

Mwenyekiti wa Taasisi ya Vyombo vya Habari Kusini mwa Afrika – Tawi la Tanzania (MISA Tanzania), Edwin Soko,katika mafunzo ya siku moja ya uandishi wa habari za amani, yaliofanyika jijini Dodoma

Mafunzo hayo ambayo yaliotolewa na MISA Tanzania kwa waandishi wa habari 100 kutoka mikoa ya Tanzania Bara na Visiwani,yalilenga kuwajengea uwezo wa namna ya kuripoti habari inayolinda amani,kupunguza taharuki na kuimarisha mshikamano wa kitaifa.

Soko,ametahadharisha kuwa uandishi unaolenga kugawa jamii unadhoofisha misingi ya amani ambayo nchi imeijenga kwa miaka mingi,huku akisisitiza kuwa vyombo vya habari vinapaswa kujikita kuandika habari ambazo zitaleta umoja na mshikamo sio kuchochea mgawanyiko na uhasama kwa taifa.

“Hii ndiyo Tanzania, sisi ndiyo Watanzania,tukiruhusu nchi yetu ikawaka moto hatuna pa kwenda.Wapo wanaolaumu na kuona kama vyombo vya habari havijatimiza wajibu wake Oktoba 29,2025 wakati wa uchaguzi, na kusahau kuwa vyombo vya habari havilengi kwenye kuiboa jamii bali kuijenga ,”amesema Soko.

Pia Soko ametumia fursa hiyo,kusisitiza umuhimu wa waandishi na vyombo vya habari kuwa uhuru na kufanya kazi zao kwa kufuata maadili ya uandishi bila msukumo au shinikizo kutoka kwa watu binafsi.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha SAUT Mwanza, Dkt. Dotto Bulendu, akizungumza wakati akiwasilisha mada kuhusu umuhimu wa uandishi wa habari jengefu,amesema jamii inahitaji taarifa zenye mizania sahihi pia sauti za vijana zishirikishwe na zisikike katika mambo ya kitaifa.

“Nadhani uandishi huu utatusaidia kuondoka hapa tulipo,wananchi wanataka kuona serikali ikiwajibika na ikija na majibu pia wanahitaji kusikilizwa. Kwa maana hiyo waandishi tunatakiwa kuwa kiunganishi cha makundi yote na kuepuka habari zinazoibua taharuki,”amesema Bulendu na kuongeza:

“Vijana wapo wazi kuhusu hisia zao,ni vizuri tukawasilikiza na kusaka suluhu ya hisia zao.Vijana hawa wapo mitandaoni ambapo kumetawaliwa na habari hasi ambazo wanasosholojia wanasema zinazalisha jamii yenye hasira, iliyokata tamaa, isiyo na majibu ya changamoto zao, iliyo tayari kwa lolote bila kupima madhara,”.

Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Dennis Londo, akizungumza wakati akifungua mafunzo ya siku moja ya uandishi wa habari za amani yaliondaliwa na MISA Tanzania na kufanyika jijini Dodoma

Kwa upande wake Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini,DCP David Misime,akiwasilisha mada ya wajibu wa vyombo vya habari katika kukuza amani amesema ni pamoja na kuandaa na kutangaza taarifa nyingi zenye maudhui ya kuhımıza na kuimarisha umoja, mshikamano, amanı,utulivu na upendo utakaowezesha maridhiano.

“Yaliyotokea Oktoba 29,2025 hakuna ambaye hakuonja machungu yake.Tumejifunza,binafsi nimejifunza namna ya umuhimu wa amani,”amesema Misime.

DCP.Misime amesema, waandishi wanapaswa kubuni na kukuza majadiliano yanayojenga badala ya kugawa wananchi na taifa,kuzingatia ukosoaji wa kihabari unaojenga na wenye lengo la kuboresha,kuripoti mapungufu bila kuchochea migogoro,kuchambua masuala kwa uadilifu pamoja na kutoa majibu mbadala.

Amesema,waandishi wa habari ni watu muhimu na wana mchango mkubwa katika kukuza na kuimarisha usalama, utulivu na amani.

Ambapo umuhimu huo unajidhihirisha katika uwezo wa kufanya tafiti za kiuandishi,kuandika kwa weledi na kusambaza taarifa sahihi, zilizotoka katika vyanzo ya kuaminika na zilizo thibitishwa zisizo egemea upande mmoja au wa kibinafsi .

“Mara zote tuangalie suala la kuunganisha watu kuwa wimbo na kipaumbele katika taarifa zetu na habari za kugombanisha na kuchochea ziwe mwiko,kuepuka kuandika na kutangaza yanayo ongeza chumi kwenye kidonda badala yake kuandika habari za kukuza majadiliano na maelewano pamoja na kuimarisha utambulisho na mshikamano wa taifa,”amesema DCP.Misime.

Akifungua mafunzo hayo Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi,Dennis Londo, amesema serikali imeweka msukumo katika kuhakikisha upatikanaji wa taarifa sahihi na uhuru wa vyombo vya habari. 

Baadhi ya washiriki wa mafunzo ya siku moja ya uandishi wa habari za amani yaliondaliwa na MISA Tanzania na kufanyika jijini Dodoma
Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini DCP.David Misime, akzungumza katika mafunzo ya siku moja ya uandishi wa habari za amani yaliondaliwa na MISA Tanzania na kufanyika jijini Dodoma