November 22, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mwenyekiti wa TAMWA Joyce Shebe akizungumza na waandishi wa habari wanawake juu ya Changamoto mbalimbali wanazokumbana nazo vyumba vya habari

Waandishi wa habari wanawake watakiwa kujituma

Na Mwandishi wetu,timesmajira,Online

WAANDISHI wa Habari wa kike nchini wameshauriwa kujituma kwa bidii na kutokata tamaa katika uandishi wao kwa lengo la kuhakikisha wanapiga hatua katika kazi zao.

Akizungumza Dar es Salaam hivi karibuni wakati wa semina ya waandishi wa habari wanawake iliyoandaliwa na Chama cha waandishi wa habari wanawake Tanzania(TAMWA) chini ya mradi wa ‘Women in Newsroom’ unaofadhiliwa na taasisi ya The Finnish Foundation for Media and Development (Vikes) juu ya waandishi wanawake wanavyofanya kazi katika vyumba vyao vya habari na changamoto wanazopitia.

Afisa Mwandamizi Idara ya Habari Maelezo,Lilian Shirima amesema, waandishi wanawake wengi wanapitia changamoto nyingi katika vyumba vya habari ikiwemo manyanyaso, kushushwa thamani na kuonekana hawawezi katika kazi hali inayowafanya kujikuta wanakata tamaa na kurudi nyuma.

Amesema, kutokana na tasnia kuzidi kuwa na wigo mpana na kufanya kazi kwa kuzingatia maadili na misingi ya taalum, waandishi wanawake wanapaswa kujitambua na kupanua fikra zao katika kazi.

“Waandishi wa habari wanawake mjitahidi kujiamini na kujituma katika kazi zenu ili kuweza kuvuka mishale mbalimbali ya kiubanguzi ndani ya vyombo vya habari vyenu hii itasaidia kuwawezesha kuwafanya mfanikiwe katika kazi zao,” amesema Afisa huyo.

Aidha amesema, waandishi hao wanapaswa kufuata sheria ya huduma ya vyombo vya habari hasa katika kipindi ambacho nchi inatarajiwa kufanya uchaguzi mkuu Oktober mwaka huu.

Mkurugenzi wa TAMWA, Rose Reuben amesema, lengo la kufanya semina hiyo ni kujenga uwezo katika kuhimili mikiki na kujenga taalum za waandishi wa habari wanawake.

Kwa upande wake, Mwandishi Mkongwe, Rose Mwalimu amesema moja ya mada ambayo amepata fursa ya kuwafundisha waandishi hao ni pamoja na umuhimu wa vyombo vya habari katika kuleta usawa wa kijinsia.