Na.Mwandishi Wetu,TimesMajira
WAANDISHI wa Habari 64 wamefuzu hatua ya mwisho ya kuwania Tuzo za Uandishi wa Habari za Maendeleo (Samia Kalamu Awards 2026). Vyombo vya habari 11 pia vimefuzu hatua hiyo.
Washindi wanatarajiwa kutunukiwa tarehe 5 Desemba 2026 katika hafla itakayofanyika kwenye Ukumbi wa Mlimani City, jijini Dar es Salaam, huku Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Dkt. Samia Suluhu Hassan, akitarajiwa kuwa mgeni rasmi.
Mkuu wa Idara ya Uhusiano na Mawasiliano kwa Umma wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Rolf Kibaja, ametangaza orodha ya waliofuzu leo katika mkutano na Waandishi wa Habari uliofanyika katika ofisi za TCRA jijini Dar es Salaam akimwakilisha Mkurugenzi Mkuu wa mamlaka hiyo, Mhandisi Peter Mwasyalanda.
Kibaja amesema jumla ya kazi 3,003 ziliwasilishwa kuwania tuzo hizo ambapo baada ya tathmini ya majaji, kazi 882 zilifuzu kupigiwa kura na umma. Katika hatua hiyo, jumla ya kura 317,399 zilipigwa.

Ameeleza kuwa waliofuzu hatua ya mwisho walipatikana kupitia tathmini ya majaji 19 na kura za wananchi. Majaji walizingatia ubora wa maudhui, uzingatiaji wa maadili ya taaluma, matumizi ya utafiti na takwimu, athari chanya kwa jamii na mchango wa kazi hizo katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Akijibu maswali ya Waandishi wa Habari, Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA), Dkt. Rose Reuben, amesema uteuzi wa washindani waliofuzu hatua ya mwisho ulizingatia ubora wa kazi zilizowasilishwa na vigezo vilivyochapishwa kwenye tovuti rasmi ya Samia Kalamu Awards 2026 wakati wa kutangaza nafasi ya kushiriki.

Dkt. Reuben amesema Kamati ya Maandalizi itawapa waliofuzu maelekezo kuhusu ushiriki wao katika hafla hiyo na kwamba orodha kamili inapatikana kwenye tovuti rasmi ya Samia Kalamu Awards.
Naye Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari (JAB), Wakili Patrick Kipangula, amewashukuru Waandishi wa Habari kwa kushiriki katika mchakato wa tuzo hizo na kuwahimiza kuzingatia maadili, weledi na uwajibikaji katika kazi zao.
Amesisitiza kuwa kutoa taarifa sahihi kwa kuzingatia viwango vya taaluma kunaimarisha imani ya jamii kwa vyombo vya habari.

Wakili Kipangula amesema tuzo hizo pia zinatoa fursa kwa Waandishi wa Habari, Maafisa Habari na vyombo vya habari kutambuliwa kwa ubora wa kazi zao zilizochapishwa au kurushwa hewani.
Samia Kalamu Awards zinaratibiwa na TCRA kwa kushirikiana na TAMWA na JAB. Tuzo hizo zilianzishwa mwaka 2024 ili kutambua na kuhamasisha ubora, weledi na ubunifu katika uandishi wa habari za maendeleo. Hafla ya kwanza ya utoaji wa tuzo hizo ilifanyika mwaka 2025. Msimu wa pili una kaulimbiu “Kalamu kwa Maendeleo.”


More Stories
Azania kutoa mikopo ya riba nafuu kwa wanawake
Nkasi yazipongeza shule zilizofanya vizuri
Uongezaji thamani Madini kupewa kipaumbele TMIC 2026