November 17, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Rufiji Basin Cup yaleta mwamko vijana kushiriki michezo Mbarali

Na Mwandishi wetu,TimesmajiraOnline,Mbeya

KUELEKEA Mashindano ya fainali ya Rufiji Basin Cup katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali mkoani Mbeya uongozi wa Taasisi isiyokuwa ya kiserikali inayojishughulisha na masuala ya mazingira(SALIOTA) umesema uwepo wa mashindano hayo kwa wananchi umepelekea kuwepo kwa mwamko mkubwa wa kujikita kwenye michezo badala ya vitendo vya uhalifu.

Kauli hiyo imetolewa Novemba 16,2026 na Elisha Mwanikawaga ambaye ni Mkurugenzi wa Shirika lisilo kuwa la kiserikali ambalo linajishughulisha na masuala ya mazingira (SALIOTA)wakati akizungumza na Timesmajira kuhusiana na mashindano ya Rufiji Basin Cup ambayo lengo lake kubwa ni kuhamasisha jamii juu ya Uhifadhi wa vyanzo vya maji na mazingira, matumizi ya nishati safi pamoja na kupinga ukatili wa kijinsia.

Mkurugenzi huyo amesema kuwa kupitia mashindano hayo kumeonyesha mwamko mkubwa wa watu kujitokeza toka mashindano hayo yalipoanza hasa makundi ya vijana ,wanawake na wazee maeneo yote ya vijijini ambako ligi ilikuwa ikiendekea .

“Mafanikio tumeona makubwa kwani ya kuelekea mwisho wa fainali bado kuna watu wanatamani ligi hiyo iweze kuendelea ,tumeona sasa wengi wamejifunza utunzaji wa vyanzo vya maji ,mazingira kupitia michezo tunaenda kuona mabadiliko makubwa sasa kwa wananchi wetu”amesema.

“Lakini kupitia mashindano haya tumewatengenezea vijana uelewa wa pamoja juu ya utunzaji wa vyanzo vya maji na pia tumeweka umoja wa kukaa pamoja vijana katika kujadili masuala ya msingi “amesema.

Hata hivyo Mwanikawaga amesema kuwa Timu ambazo zimeingia fainali ni Azimio Mswiswi kutoka kata ya Kongolo baada ta kumtoa Igunda Muungano kwa goli 2_1, na Timu nyingine iliyoingia fainali ni Isunula kutoka kata ya Mawindi iliyomtoa Mwakaganga kwa goli 3_1.

Kwa upande wake Mratibu wa Miradi wa shirika lisilokuwa la kiserikali la SALIOTA,Robert Eliah amesema kuwa mashindano hayo yalipoanza yalikuwa chini lakini wananchi wameendelea kuwa na mwamko mkubwa hususan kundi la vijana mabadiliko yatakuwa makubwa baada ya mashindano haya.

“Mwanzo tulikuwa tunatumia nguvu kubwa lakini sasa mwitikio ni mkubwa mpaka imefika hatua wananchi wanauliza vipeperushi vya kutoa elimu ya utunzaji vyanzo vya maji na mazingira sasa elimu hii imefika mbali “

Fainali ya Ligi ya rufiji basi cup inatarajiwa kuhitimishwa Novemba 18 mwaka huu katika viwanja polisi wilayani Mbarali mkoani Mbeya ambapo washindi watapata zawadi mbalimbali na kukabidhiwa Kombe.