Daud Magesa, Timesmajira Online, Mwanza
WANACHAMA wa Chama Cha Mapinduzi (CCM),Kata ya Mabatini, Wilaya ya Nyamagana,mkoani Mwanza,wameadhimisha miaka 48 ya kuzaliwa kwa chama hicho kwa kupanda miti 245 katika taasisi za umma.
Akizungumza na Timesmajira Online,Leo wakati wa zoezi la kupanda miti hiyo , Mwenyekiti wa CCM Kata ya Mabatini, Paul Yomola,amesema katika madhimisho hayo wamemua kupanda miti ya matunda na vivuli katika shule ya Sekondari Mtoni,shule za Msingi Mabatini A na B, ili kulinda,kutunza mazingira na kurejesha uoto wa asili.
Pia,upandaji miti huo wameufanya ili kuunga mkono jitihada za Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan,katika utunzaji wa mazingira nchini ambaye ni kinara wa kuhamasisha utunzaji wa mazingira Afrika.
“Kupanda miti 245 ni hatua nzuri ya kuhamasisha utunzaji wa mazingira pia,inaendana na juhudi za Rais Dk.Samia, katika kuhamasisha Afrika kutunza mazingira ikizingatiwa mazingira ni kila kitu katika maisha ya binadamu,”amesema Yomola na kuongeza:
“Katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi,ni muhimu kuyalinda na kuyatunza yawe salama na endelevu kwa vizazi vya sasa na vijavyo kwani tusipoyalinda yatatuadhibu.Miti hii tulioipanda hakikisheni mnaitunza ili kuboresha mazingira na uoto wa asili,”.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Mabatini Kusini, Hamisi Nassoro, amesisitiza kuwa mabadiliko ya tabianchi ni changamoto inayosumbua Dunia kwa sasa, hivyo jamii ina jukumu la kushiriki kikamilifu katika upandaji miti na kulinda mazingira.
Pia,Ilani ya CCM imeendelea kusisitiza umuhimu wa utunzaji wa mazingira na kupanda miti kama suluhisho la kukabiliana na athari za uharibifu wa mazingira na mabadiliko ya tabianchi.
More Stories
Waislamu wamuombea dua Rais Samia,wasisitiza umoja
Samia: Serikali imejifunza somo kuporomoka ghorofa
Wanachama CCM Kata ya Rujewa wajitokeza kufanya usafi kituo cha afya