Na Mwandishi Wetu, Zanzibar
WAKATI vuguvugu la uchaguzi mkuu likiendelea kushika kasi Visiwani Zanzibar, Chama cha Wananchi (CUF) kimedai kubaini mkakati mzito wa kupandikiza viongozi ndani ya chama hicho unaoratibiwa na waliowahi kuwa viongozi wa chama hicho.
Habari za kuaminika kutoka vyanzo mbalimbali vya duru za kisiasa visiwani humo, vimeliambia Majira kuwa waliokuwa viongozi wa CUF Zanzibar wamefanikiwa kupandikiza viongozi ndani ya chama hicho Zanzibar na kusababisha kuzorota kwa shughuli za ujenzi wa CUF.
Chanzo hicho kimeeleza kwamba mbinu zinazotumika kwa sasa kuizofisha CUF ni kuwatumia baadhi ya viongozi wakubwa wa upande wa Chama visiwani humo.
“Kuna maelekezo kutoka kwa viongozi wa zamani wa CUF waliohama vyama vingine kwa lengo la kuhakikisha CUF inakosa utulivu na hivyo kupelekea kukosa wagombea wa nafasi za urais, ubunge, uwakilishi na udiwani kwenye Uchaguzi Mkuu,” kilidai chanzo hicho na kueleza;
“Mtu akija Unguja na Pemba atabaini hali hiyo ambayo ipo wazi na muda si mrefu jambo hili litadhihirika mbele ya jamii ya Zanzibar na Bara kwa ujumla wake baada ya kuwepo kwa malumbano ya kisiasa baina ya wafuasi wa ACT-Wazalendo na CUF, huku kila upande ukilaumu upande wa mwingine kuwa wasaliti wa demokrasia.”
Vyanzo vyetu vimeeleza kwamba Chama cha ACT-Wazalendo kimekuwa kikiwalaumu wanachama waliobaki CUF kwamba wanaisaliti Zanzibar, wakati wana CUF wanalalamika kuwa ACT-Wazalendo kuwa imewaletea viongozi mamluki kwa lengo la kuiua CUF na historia ya harakati za ukombozi wa kweli uliopelekea mauaji ya Januari 26/27 Mwaka 2001.
Msuguano mkali baina ya CUF na ACT-Wazalendo kwa upande wa Zanzibar unazidi kuongezeka kadri uchaguzi unavyokaribia, kila chama kikijiona kina haki kubwa ya kuwatetea wananchi wa Zanzibar kuliko kingine.
Hatua ndiyo imeibua mkakati wa kile kinachodaiwa baadhi viongozi wa CUF Zanzibar kutuhumiwa kupokea maelekezo ya utendaji wa shughuli za Chama kutoka kwa viongozi wa ACT Zanzibar.
Hata hivyo mtoa habari wetu amedokeza kwamba upande wa ACT-Wazalendo nako kuna malalamiko kutoka kwa wanachama wake baada ya Mansour Yusuph Himid kutangaza nia ya kugombea nafasi ya Urais kupitia Chama hicho, jambo ambalo linapingwa na wanachama nguli wa zamani wa Chama hicho kwa madai kuwa, Himid sio tu mgeni bali pia ni miongoni mwa waliokuwa wajumbe wa Baraza la Mapinduzi waliohusika na manyanyaso mengi dhidi ya Wazanzibar.
Baadhi ya viongozi wa CUF walipoulizwa kuhusiana mtifuano huo, wamesema taarifa hizo zinaweza kuwa na ukweli au pia zikawa ni propaganda za kisiasa wakati huu wa kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Urais, Ubunge, Uwakilishi na Udiwani.
“Hatutegemei kuingia kwenye mgogoro mwingine utaokaonekana ni hujuma za ACT badala ya ule wa Maalim ambao umedumu kwa miaka mitatu mahakamani,” amesema mmoja wa viongozi akizungumza kwa sharti la jina lake kutochapishwa gazetini.
Amesema ingawa kwenye siasa panaweza pakawa na ukweli wa hilo, lakini kwa sasa hawawezi kusema lolote kwa kuwa halijajitokeza wazi.
“Tutakabiliana nalo wakati muafaka ukifika kwa sasa nguvu zetu tunaelekeza kwenye uchaguzi,” amesema.
More Stories
TTCL yafanya maboresho katika huduma zake
HGWT yawataka wazazi na walezi kulinda watoto dhidi vitendo vya ukatili
ACT-Wazalendo,waitaka Polisi kutobeba chama kimoja