December 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mkurugenzi wa Uchaguzi wa ZEC,Thabit Idarous Faina akimkabidhi Sera ya Ushiriki wa Makundi Maalum wakati wa uchaguzi Makamu Mwenyekiti wa Ushiriki Tanzania Zanzibar Salma Saadat.

Vyama vya Siasa vyatakiwa kusaidia makundi maalum katika Uchaguzi Mkuu

Mwandishi Wetu, TimesMajira Online, Zanzibar

MKURUGENZI wa Uchaguzi wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Thabit Idarus Faina amevitaka Vyama vya siasa nchini kuhamasisha ushiriki wa makundi maalum katika uchaguzi Mkuu unaotajia kufanyika Oktoba mwaka huu

Pia amezitaka Asasi za kiraia kuhamasisha mambo mawili ili wanawake washiriki katika siasa, ikiwemo hatua ya kuwaondolea woga pindi ya Mchakato mzima wa uchaguzi na kuwawezesha kifedha ili wakagombee katika majimbo wanayoona wataweza kushiriki.

Faina ameyasema hayo jana wakati alipokutana na Jukwaa la Katiba Tanzania, (JUKATA) chini ya mwamvuli wa Ushiriki Tanzania amesema wao sio jukumu lao la kuhamasisha makundi maalum kushiriki uchaguzi bali ni Vyama vya siasa.

Faina amesema, ZEC haina uwezo wa kutengeneza mazingira ya ushiriki wa makundi maalum ndani ya vyama vya siasa bali vyama hivyo viwajibike kwa kuwateua wanawake, vijana na watu wenye ulemavu katika nafasi mbalimbali.

“Katika uchaguzi mkuu ujao, tunataka muwasaidia wanawake, kwanza waondoe woga na pia kuwe na mfuko maalum ambao utawasaidia kupata fedha za kufanya kampeni, wengi wao hawana uwezo wa kiuchumi,” amesema na kuongeza kuwa

“Bila kufanya hayo, asilimia ya ushiriki wa wanawake katika ubunge, baraza la wawakilishi na udiwani, itabaki ile ile asilimia 40,” amesema Faina

Amesema vyama vya siasa ndivyo vimekuwa na udhaifu wa kuchapgua wanawake kushika nafasi ndani ya vyama au nje akatolea mfano wawakilishi katika kamati za tume ya uchaguzi visiwani humo.

“Tuna vyama 19 lakini katika kamati za tume zilizo chini ya ZEC, kuna wanawake watatu tu, ambao pia wametoka katika vyama vidogo na si vyama vikubwa vyenye majina, licha ya kuwaambia wateue wanawake katika nafasi hizo” amesema

Akizungumza katika mkutano huo, Deus Kibamba amesema JUKATA chini ya uratibu wa Ushiriki Tanzania, walikwenda kushauriana na ZEC juu ya namna bora ya kuwezesha ushiriki wa makundi maalum.

“Ingawa kuna ibara za katiba na vifungu vya sheria pamoja na kanuni, ambavyo vinazuia ubaguzi wa makundi maalum, utekelezaji wake umekuwa ni hafifu na hivyo ZEC ina uwezo wa kushadidia ushiriki wa makundi hayo katika uchaguzi mkuu ujao,” amesema

Kibamba amesema ni vyema kwa ZEC, kuboresha mfumo wake wa unasaji taarifa ili kuwezesha upatikanaji wa takwimu zinazobainisha ushiriki wa makundi hayo maalum.