December 26, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Vyama vya Siasa vyatakiwa kuepuka migogoro 

Na Bakari Lulela, Timesmajira Online

VYAMA vya Siasa nchini vimetakiwa  kuepuka migogoro ya kisiasa ambayo huleta mifarakano ndani ya taifa kwa ujumla.

 Agizo hilo limetolewa  l Julai 9,2024 jijini Dar es Salaam na Msajili wa Vyama Vya Siasa Nchini Jaji Francis Mutungi  wakati akifungua mafunzo ya siku mbili kwa viongozi wa vyama vya siasa nchini yakiwa na   lengo la kuwajengea uwezo juu ya  mabadiliko ya mfumo wa uendeshaji wa vyama hivyo pamoja na namna ya kuhimili migogoro inayotokea wenyewe kwa wenyewe pasipo kufikishana katika vyombo vya sheria .

 Jaji Mutungi amesema vyama vya siasa ni taasisi hivyo vinapaswa kusajiliwa na kutenda majukumu yanayotambulika kidemokrasia na kuachana na vurugu ambazo zinasababisha vyama hivyo kuwa na mpasuko.

 “Haya Mafunzo yatasaidia kuepukana na mambo mbalimbali ikiwemo migogoro ya ubadhilifu wa fedha za chama na matumizi mabaya ya fedha za chama hali ambayo imekua ikiripotiwa mara kwa mara kwenye taarifa ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG),’amesema Jaji Mutungi.

 Aidha, amevitaka vyama vya siasa kuwa vinara wa kujenga nchi na kwamba Tanzania sio nchi ambayo inapata utawala kwa mabavu bali ni demokrasia iliotukuka.

 “Mkifanya mema wafuasi wengi watawafuata,mkifanya maovu hakuna atakaewafuata,naomba sana nitoe wito kwenu muwambie wafuasi wenu waepukanae na migogoro na badala yake walinde amani na utulivu wa Taifa,”amesisitiza Jaji Mutungi

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Chama cha ACT – Wazalendo Ado Shaibu amesema kuwa migogoro ya vyama vya siasa inapaswa kutatuliwa kwa njia ya maridhiano na sio kutumia nguvu zisizofaa.

 “Ni kweli migogoro inapasua vyama ,hivyo ni vyema vyama kuitatua kwa njia ya maridhiano, tunaishukuru ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa kutuletea mafunzo haya ili kuondokana na migogoro kwenye vyama vyetu vya siasa,”amesema Katibu Mkuu huyo wa Act Wazalendo.

Naye, Mwenyekiti Taifa wa Chama cha Demokratic Part (DP) Philipo Fumbo amebainisha kuwa vyama vingi vya upinzani havina ruzuku kutoka serikalini hali ambayo inachangia  kushindwa kuajiri wahasibu na maofisa ununuzi hivyo kusababisha migogoro ndani ya vyama kutokana na matumizi mabaya ya fedha.

 Mafunzo ya siku mbili kwa viongozi wa Vyama vya Siasa yamelenga katika maeneo mbalimbali ikiwemo kujifunza kuandaa taarifa ya fedha ya kuwasilisha kwa CAG,pamoja na kuandaa matamko ya mali  za chama hadi kufikia kilo Septemba Mwaka huu.