December 28, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Vyama vya michezo vyatakiwa kuwasilisha mikakati yao BMT

Na Shamimu Nyaki-WHUSM, Dodoma

KATIBU Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Hassan Abbasi
ameiagiza Idara ya Maendeleo ya Michezo nchini kuhakikisha kila Shirikisho na vyama vya michezo vinawasilisha Mpango Mkakati wake katika Baraza la Michezo la Taifa (BMT).

Mikakati hiyo inatakiwa kuambatanishwa na kalenda ya mwaka ya matukio mbalimbali ya kila Chama kuanzia ngazi za kitaifa, kimataifa pamoja na timu ya Taifa .

Dkt. Abbasi amesema kuwa, lengo la kutoa agizo hilo ni kuhakikisha kunakuwepo na uelewa wa pamoja kwa wadau wote utakaoleta mafanikio zaidi katika sekta hiyo.

Amesema, lazima Taifa liwe na ushiriki wa mashindano ya michezo ambao utaleta tija, hivyo Idara hiyo ina jukumu la kuhakikisha mashindano yote ambayo nchi inashiriki katika ngazi mbalimbali yanakua na manufaa.

Mbali na agizo hilo, pia Idara hiyo imetakiwa kukutana na wadau wa sekta hiyo
wakiwemo Mashirikisho ili kubadilishana utaalamu wa namna ya kuendesha michezo kwa pamoja na kutoa ushauri wa kisera kwa wadau hao.

“Ni lazima mkutane na wadau wenu ili mjue wana mawazo gani katika sekta hii na nyie mtoe ushauri wa kitaalamu ambao utaleta tija. Ni lazima muwaeleze wadau Sera ya Michezo inasemaje kwa sababu nyie ndio mnaoisimamia sekta hii,” amesema Dkt. Abbasi.

Pia Kiongozi huyo ameahidi ushirikiano kati ya Tanzania Bara na Zanzibar katika sekta ya michezo unaendelea kuimarika ikiwemo kuimarisha Kombe la Mapinduzi.

“Muungano wetu ni muhimu na Kombe la Mapinduzi ni moja ya njia ya kutuunganisha
na kuimarisha Muungano wetu, hivyo nitoe rai kwa Vilabu kupeleka timu bora katika mashindano hayo,” amesema Dkt. Abbasi.

Akiongelea kuhusu miuondombinu ya michezo ikiwemo ujenzi wa viwanja, Dkt. Abbasi ameeleza kuwa, Serikali inaendelea kuwekeza na matarajio ni kuwa na viwanja bora vya michezo nchini na tayari Ujenzi wa Uwanja wa Dodoma umefikia

Pia ameweka wazi kuwa, mashindano ya UMITASHUMTA na UMISETA ni mashindano ambayo yanapaswa kupewa kipaumbele kwa kuwa yanazalisha vipaji vingi vya michezo mbalimbali nchini hivyo, Idara ya Michezo ina jukumu la kusimamia mashindano hayo kwa kushirikiana na wadau wengine ikiwemo TAMISEMI na Wizara ya Elimu ili vijana wanaofanya vizuri waendelezwe kupitia Chuo cha Maendeleo ya Michezo Malya pamoja na sehemu nyingine.