March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Vurugu baada zilizotokea katika uchaguzi na baada ni somo kwa Watanzania

*Viongozi wa dini ya kiislamu Mwanza wasisitiza amani idumishwe

Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online-Mwanza

Baadhi ya viongozi wa Dini ya Kiislamu mkoani Mwanza wamesema kuwa vurugu zilizotokea wakati na baada ya uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 29,2025,ni funzo kwa Watanzania wote kuhusu thamani ya amani, wajibu wa kuilinda nchi, kudumisha umoja na kuendelea kuwa watiifu kwa mamlaka halali.

Viongozi hao wameyasema hayo katika dua maalumu ya kuiombea nchi amani, iliyofanyika msikiti wa Sheikh Abubakary Zuber Bin Ally, jijini Mwanza. Wamesema chanzo kikuu cha machafuko hayo ni ukosefu wa imani, uvumilivu na heshima kwa mamlaka, mambo ambayo yamekuwa yakihatarisha mshikamano wa kitaifa.

Sheikh wa Mkoa wa Mwanza, Alhaj Hassani Kabeke, amesema vurugu hizo zimetokana na watu walio nje ya nchi kuwajaza vijana sumu ya chuki, hali iliyochochea vurugu na kuhatarisha utulivu wa taifa.

Akitaja mambo sita muhimu ya kuzingatia ili kudumisha amani ambayo ni kuhifadhi nafsi, kulinda mali, dini, heshima au cheo cha mtu, uadilifu na nchi, Sheikh Kabeke amesema kuwa mambo hayo yote yanafanyika pale ambapo kuna amani.

“Haki hupatikana pale tu panapokuwepo amani. Tulichoona siku tatu zilizopita ni hali ambayo mataifa mengi duniani hukumbana nayo, na mara nyingi matatizo hayo yakitokea huwa hayarudi nyuma kirahisi. Ni wajibu wetu kuendelea kuiombea nchi yetu amani na kuwaombea askari wetu ulinzi na usalama,” amesema Sheikh Kabeke.

Amewataka Watanzania kuendelea kuwalea vijana katika misingi ya maadili mema, kuachana na chuki na wivu, na kuendelea kumuombea Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan,ili aendelee kuongoza nchi kwa amani na umoja.

Kwa upande wake, Sheikh wa Bilal Muslim Kanda ya Ziwa,Hashim Ramadhan,amesema vurugu na taharuki zilizojitokeza ni matokeo ya baadhi ya Watanzania kukosa imani na uvumilivu.

“Baadhi yetu tumekuwa tukihamasishwa na watu wasioitakia mema nchi yetu, hasa wanaoishi nje ya nchi. Wanaeneza chuki na ghasia wakidai nchi ‘inaliwa’, huku wakichochewa na mataifa ya Magharibi yanayotuonea wivu kwa kuwa sisi ni kisiwa cha amani,”amesema Sheikh Ramadhan.

Naye Sheikh wa Wilaya ya Misungwi, Hussein Hussein,amesema kabla ya uchaguzi viongozi wa dini walimwomba Mungu kwa ajili ya amani, na kwamba Waislamu wanapaswa kuendelea kuzingatia maelekezo ya Qur’an badala ya kufuata mambo yasiyo na msingi.

“Qur’an inatuelekeza kuwatii viongozi wetu. Oktoba 29, 2025 tulifanya uchaguzi vizuri, lakini saa 10:30 usiku ghafla vurugu zikaanza baada ya vijana kujikusanya na kuharibu mali za watu na miundombinu ya serikali. Dua hii ni ya kumwomba Mungu atusamehe,” alisema Sheikh Hussein.

Aidha, Mjumbe wa Baraza la Masheikh Wilaya ya Nyamagana, Ayub Khatibu, alisema vurugu hizo zilitokana na kukaidi maelekezo ya serikali na viongozi wa dini, akiwataka Watanzania kuendelea kulinda amani na kutii mamlaka.

Sheikh wa Wilaya ya Ilemela, Abdulwarith Jumaa, alisema mkusanyiko huo wa dua ni ishara ya heri na amani, akisisitiza kuwa hakuna jambo lolote linaloweza kufanyika bila utulivu.

“Haya yanayotokea ni kutuonya kuhusu kutoandamana hovyo. Tuna wajibu wa kumuunga mkono Rais Samia. Mungu anatukumbusha kuhusu amani katika Qur’an, Sura ya 15, pale Ibrahim aliposema: ‘Mungu, ujalie mji huu wa Makka uwe wa amani, nilinde mimi na kizazi changu tusije tukaabudu masanamu,”amesema Sheikh Jumaa.

Naye Kadhi wa Wilaya ya Nyamagana, Sheikh Fadhil Ndumiwe, alionya kuwa kutomtii kiongozi ni kujitafutia matatizo, akisema kuwa uasi huleta madhara makubwa kwa mtu na jamii.

“Ukimwasi Mungu unapata dhiki. Ukianzisha vurugu, je, unaweza kuishi kwa amani? Tuhamasishane kuzuia wanaotaka kuvuruga nchi, maana Rais Dk. Samia hajatuamrisha kufanya maovu. Tumuunge mkono kwa nia yake njema ya kuwatumikia Watanzania,” amesema Kadhi Ndumiwe.