Na Agnes Alcardo, Timesmajira Online, Dar es Salaam
KAMPUNI ya Vodacom Tanzania, imezindua rasmi kampeni mpya inayojulikana kama ‘Sambaza Shangwe, Gusa Maisha’ yenye lengo la kuwazawadia wateja wake zawadi mbalimbali.
Kuelekea msimu wa sikukuu kampuni hiyo imedhamiria kutoa zawadi ikiwemo bima ya afya kwa mama na mtoto Tanzania bara na Visiwani.
Akizungumza wakati wa kuzindua kampeni hiyo jijini Dar es Salaam leo, Mkurugenzi wa Biashara na Masoko wa Vodacom Tanzania, Linda Riwa amesema msimu huu wa sikukuu utakuwa wa kipekee.
Amesema, wanatarajia kuendesha promosheni kabambe zinazolenga kuwazawadia wateja wa Vodcom pia watatoa bima ya afya kwa watoto watakaozaliwa mwezi wa Disemba 2023 pamoja na mama zao.
“Kampeni ya ‘Sambaza Shangwe, Gusa Maisha’ iliyozinduliwa leo inatarajiwa kudumu kwa takribani wiki 10 mpaka katikati ya mwezi Januari 2024.
“Mwezi Novemba kampeni hii itajikita katika kuwazawadia na kuwakabidhi wateja zawadi mbalimbali, na mwezi Disemba itatumika mahususi kwa kutoa zawadi ya upendo ya bima kubwa ya afya kwa mama na mtoto,” amesema Linda.
Ametoa wito kwa wananchi kujiunga na vodacom ili waweze kujipatia fursa zinazotolewa na Kampuni hiyo.
Naye Mkurugenzi wa M-Pesa, Epimack Mbeteni amesema Vodacom inatambua kuwa katika msimu wa sikukuu Watanzania wengi hufanya manunuzi na malipo ya huduma mbalimbali.
“Vodacom inawahimiza kufanya miamala hiyo kupitia njia za kidigitali haswa M-Pesa kwani ni rahisi na salama zaidi.
“Vile vile, kadri wateja wanavyofanya miamala kwa njia hii ndivyo wanavyojiongezea nafasi ya kujishindia zawadi za papo kwa hapo au zile zitakazotolewa kupitia droo za kila wiki,” amesema.
More Stories
Elon Musk : Bill Gates atafilisika endapo…
CRDB yazindua matawi Majimoto, Ilula kuwahudumia wananchi
Lina PG Tour yafufua gofu Moshi