May 3, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mhagama azindua Wiki ya Vijana, WCF kulinda nguvu kazi ya vijana

NA K-VIS BLOG, MANYARA

Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa, amewataka viongozi wote nchini, kuwatambua vijana wabunifu na kuhakikisha wanaendelezwa katika ubunifu wao.

Ameyasema hayo katika hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Mhe. Jenista Mhagama, wakati wa uzinduzi wa Wiki ya Vijana Kitaifa, kwenye viwanja vya CCM, Stendi ya zamani mjini Babati, Oktoba 10, 2023.

Alisema, Vijana wanafanya asilimia 56.6 ya nguvu kazi ya taifa, hivyo ni vizuri viongozi, mfuko wa vijana na taasisi za kifedha zikasaidia kuwaibua vijana hao ambao sasa wako mil. 21.3 nchi nzima.

“Serikali ina kila sababu ya kuwapongeza vijana, mataifa mengi yaliyoendelea na nchi ambazo zimekuwa kwenye uchumi wa viwanda, walianza na viwanda vidogo vidogo, kama hivi ambavyo vijana wetu wamedhihirisha kwenye wiki hii ya Vijana, na sote tumeshuhudia.” Alisema.

Wiki hiyo ambayo itafikia kilele Oktoba 14, 2023, inaadhimishwa kwa maonesho ya shughuli mbalimbali zinazotekelezwa na vijana, lakini pia taasisi wezeshi zilizo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu pamoja na taasisi binafsi.

Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), ni miongoni mwa taasisi ambazo ziko chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu na unashiriki kwenye maonesho hayo yanayokwenda sanjari na maadhimisho ambapo lengo kuu la WCF ni kulinda nguvu kazi kwa kulipa fidia kwa wafanyakazi wanoumia, kuugua ama kufariki kutokana na kazi ambapo wanufaika wakubwa ni vijana.

Kwa upande wake, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Mhe. Profesa Joyce Ndalichako, alisema, Wiki ya Vijana inalenga kutambua mchango wa waasisi wa taifa hili, Hayati Babab wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, na Sheikh Abeid Aman Karume, ambao walilipigania taifa wakiwa bado vijana kabisa.

“Wiki hii inaenda sambamba na sherehe za kilele cha mbio za Mwenge wa Uhuru na ibada ya Kumbukumbu ya hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na imewaleta pamoja vijana kutoka pande zote mbili za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Bara na Zanzibar ili kubadilishana uzoefu wa shughuli wanazozifanya na kuonyesha ubunifu wa kazi wanazozifanya.” Alifafanua Profesa Ndalichako.

Akizungumzia ushiriki wa WCF kwenye Wiki ya Vijana, Mkurugenzi Mkuu wa WCF Dkt. John Mduma, amesema, lengo la WCF ni kulinda nguvu kazi kubwa ya taifa na kama mnavyofahamu kijana ndiyo nguvu kazi ya taifa.

Alisema, Mfuko unatoa mafao yanayomnufaisha moja kwa moja kijana hivyo kuendelea kuunga mkono jitihada za serikali za kuwekeza katika vijana walioko katika sekta mbalimbali.

“WCF hutoa mafao ya fidia kwa vijana yanayo rejesha uwezo wao wa kumudu maisha, na wafanyakazi hawachangii katika Mfuko huu, bali wachangiaji ni waajiri peke yao.” Aliongeza. Dkt. Mduma.

Akifafanua zaidi, Dkt. Mduma, alisema, pale ambapo mfanyakazi ataumia au kupata ugonjwa unaotokana na kazi, basi Mfuko utagharamia matibabu yake kwa asilimia mia moja (100%), kwa kipindi chote ambacho yuko katika matibabu.

Alisema, WCF inahakikisha kijana hapotezi kipato kwa kutoa fao la ulemavu wa muda mfupi ambapo atalipwa sehemu ya mshahara wake kwa siku zote ambazo hawezi kuzalisha kipato.

“Kwa kuzingatia maslahi ya vijana na wategemezi wao WCF inatoa msaada wa mazishi pale ambapo mtu atafariki kutokana na kazi. Wategemezi ambao ni wajane au wagane hulipwa pensheni kwa kipindi chote cha maisha yao na watoto hulipwa hadi wanapofikisha miaka 18 au zaidi iwapo wako masomoni.” Alibainisha

Alisema Mfuko, umewekeza katika sehemu mbalimbali ikiwemo kwenye viwanda ambapo vijana wameweza kupata fursa za ajira, biashara na kujipatia kipato.

Wiki hiyo imebeba kauli mbiu isemayo “Vijana na Ujuzi Rafiki wa Mazingira kwa Maendeleo Endelevu.”

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Mhe. Jenista Mhagama, akizungumza jambo na wafanyakazi wa WCF, alipotembelea banda la Mfuko huo, Oktoba 10, 2023.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Mhe. Jenista Mhagama, akizungumza wakati wa uzinduzi wa Wiki ya Vijana Kitaifa kwenye viwanja vya CCM, Stendi ya zamani Mjini Babati, Manyara, Oktoba 10, 2023.


Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Mhe. Profesa Joyce Ndalichako, akizungumza wakati wa uzinduzi wa Wiki ya Vijana Kitaifa kwenye viwanja vya CCM, Stendi ya zamani Mjini Babati, Manyara, Oktoba 10, 2023.
Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Mhandisi Cyprian Luhemeja (wapili kushoto), Mkurugenzi Mkuu wa WCF, Dkt. John Mduma (wakwanza kushoto), wakiwa kwenye picha ya pamoja na wafanyakazi wa WCF, kwenye banda la Mfuko huo kwenye viwanja vya CCM, Stendi ya zamani. mjini Babati, Manyara, Oktoba 12, 2023
Mzee Joseph Butiku (katikati) akiwa kwenye picha ya pamoja na Mkurugenzi Mku wa WCF, Dkt. John Mduma (kulia) na Mshereheshaji maarufu nchini, Mzee Peter Mavunde, kwenye banda la Mwalimu Nyerere Foundation kwenye viwanja vya CCM, Stendi ya zamani mjini Bababti, Mkoani Manyara leo Oktoba 12, 2023.
Mkurugenzi Mku wa WCF, Dkt. John Mduma (katikati) akiwa kwenye picha ya pamoja na wafanyakazi wa WCF, wanaotoa huduma kwenye banda la Mfuko huo, wakiongozwa na Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano, Bi. Laura Kunenge, (wapili kushoto mbele).
Elimu ya Fidia kwa Wafanyakazi ikitolewa kwenye banda la WCF