November 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Viziwi wapatiwa elimu ya usalama barabarani

Judith Ferdinand, Timesmajira Online, Mwanza

Ili kudhibiti ajali kwa makundi yote ikiwemo maalumu Kitengo cha Usalama Barabarani Mkoa wa Mwanza kimetoa elimu ya usalama barabarani kwa viziwi.

Elimu hiyo imetolewa na Koplo, Rehema Makalla wa Kitengo cha Elimu Usalama Barabarani Mkoa wa Mwanza akiwa pamoja na Mtafsiri wa lugha za alama, Naibu Katibu wa Baraza la Usalama Barabarani (RSA) Mkoa wa Mwanza, Subira Sabi katika maadhimisho ya Wiki ya Viziwi yaliyofanyika kwenye ukumbi wa Mkuu wa mkoa wa Mwanza.

Lengo la elimu hiyo ni kufikisha ujumbe kwa makundi yote ili kuwa makini wanapotumia barabara na kupunguza ajali zinazoweza kuepukika.

Kwa upande wake Mkuu wa Dawati la Elimu ya Usalama Barabarani Mkaguzi Msaidizi wa Jeshi la Polisi Charles Munthal ametumia barabara ya mfano wa Jiji la Mwanza kufikisha elimu hiyo kwa wakazi wa Jiji hilo.

Maadhimisho hayo kitaifa yatafanyikia mkoani Mbeya kuanzia Septemba 25 hadi 30 mwaka huu kauli mbiu ikiwa ‘Viziwi popote walipo Duniani wanauwezo wa kutumia lugha ya alama’.