Na Waandishi Wetu, TimesMajira Online
MECHI za Ligi Kuu Tanzania Bara (VPL) zinaendelea kuchezwa leo katika viwanja vinne tofauti baada ya kumalizika kwa mapumziko ya siku kadhaa kupisha mchezo wa kimataifa wa kirafiki wa timu ya Taifa ya Tanzania.
Katika uwanja wa Kaitaba, Bukoba, wenyeji Biashara United ambao wanashika nafasi ya sita katika msimamo wa Ligi wakiwa na pointi 10, watawakaribisha Ihefu katika mchezo utakaochezwa saa 10:00 jioni ambao wanataka kujinasua katika nafasi za chini.
Hadi sasa katika mechi tano walizocheza, timu hiyo inayoshika nafasi ya 17 imejikusanyia alama tatu baada ya mechi moja dhidi ya Ruvu Shooting huku wakipoteza dhidi ya Simba, Mtibwa Sugar, Mwadui na Gwambina.
Katika uwanja wa Jamhuri, Dodoma kutakuwa na vita ya Maafande itakayowakutanisha wenyeji JKT Tanzania watakaowakaribisha Ruvu Shooting.
Mchezo huo unatarajiwa kuwa na ushindani mkubwa kutokana na timu zote mbili kupoteza mechi zao zilizopita katika uwanja huo ambapo Ruvu Shooting walifungwa goli 2-0 na Dodoma Jiji huku JKT wakifungwa goli 4-0 na Simba.
Kagera Sugar watakuwa ugenini kuwakabili wenyeji wao Namungo FC katika mcheso utakaochezwa kwenye uwanja wa Majaliwa Lindi.
Namungo wanarudi tena katika uwanja wao wa nyumbani huku wakitaka kurekebisha makosa waliyoyafanya katika uwanja huo baada ya kufungwa goli 1-0 katika mchezo wao uliopita dhidi ya Mwandui.
Katika uwanja wa Uhuru Dar es Salaam, wenyeji KMC wameapa kuwanyoosha wapinzani wao Coastal Union katika mchezo utakaochezwa saa 10:00 jioni.
KMC wanataka kutumia mchezo huo kurekebisha makosa ambayo yaliwafanya kudondosha alama sita katika mechi zao mbili zilizopita dhidi ya Kagera Sugar na Polisi Tanzania.
More Stories
Bei za mafuta Novemba 2024,zaendelea Kushuka
TARURA yaomba Mkandarasi aitwe
Ilemela yakusanya bilioni 3.7.robo ya kwanza