Na Doreen Aloyce,TimesMajiraOnline,Dodoma.
WIZARA ya Uwekezaji,Viwanda na Biashara
imewataka wazalishaji wa bidhaa zote za viwandani kuongeza jitihada za uzalishaji wa bidhaa kwa ubora unaohitajika sokoni na kwa kufuata Sheria, Kanuni na Taratibu zilizowekwa ili kukabiliana na mfumuko wa bei za bidhaa mbalimbali.
Pia imetoa majibu juu ya malalamiko ya watuamiaji wa bidhaa ya Saruji aina ya Hauxin inayozalishwa na kiwanda cha Maweni Limestone Limited kilichopo Mkoani Tanga kuhusu upungufu wa uzito wa bidhaa hiyo.
Majibu hayo yametolewa jijini hapa leo,April 13,2023 na Naibu Waziri wa Wizara hiyo,Exaud Kigahe wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mwenendo wa bei za mazao ya chakula na bidhaa muhimu nchini kwa mwezi Machi hadi Aprili mwaka huu ambapo amesema kwa mujibu wa kifungu namba 41(a) na (b) cha sheria ya Vipimo, Sura ya 340, kinatoa katazo kwa mtu yeyote kuuza bidhaa yoyote iliyo chini ya uzito, kipimo au namba kama inavyohitajika kwa mujibu wa Sheria.
“Sheria hii pia inatoa katazo kwa mtu yeyote katika ufanyaji biashara kutoa taarifa za uongo juu ya bidhaa yoyote kuhusu uzito, kipimo, namba, geji au kiwango. Endapo makosa haya yatafanyika wote watakuwa wametenda kosa kwa mujibu wa Sheria hii,”amesema.
Amefafanua kuwa kwa upande wa mwenye duka anajukumu la kuhakiki kila bidhaa anayouza kabla ya kumuuzia mlaji wa mwisho na kujiridhisha kuwa bidhaa husika ipo katika hali inayotakiwa kulingana na matakwa ya Sheria hivyo Sheria hiyo ya Vipimo sura ya 340 inatoa adhabu mbili kwa mtu ambaye atakuwa ametenda makosa.
“Endapo mtu huyo atakuwa amekiri kosa, Sheria imempa mamlaka Kamishna wa Wakala wa Vipimo kufifisha kosa (compounding of offences) na kumtoza faini mtu huyu ya kiasi kisichopungua shilingi laki moja na kisichozidi Milioni ishirini, hii ni kwa mujibu wa kifungu cha 46 cha Sheria ya Vipimo kama kilivyofanyiwa marekebisho na kifungu cha 48 cha Sheria ya marekebisho mbalimbali ya Sheria Na. 3 ya mwaka 2016.
“Sheria hii imetoa adhabu ya jumla kwa mtu ambaye atakuwa ametenda kosa chini ya sheria hii na ni mkosaji wa mara ya kwanza akitiwa hatiani Mahakamani basi atawajibika kulipa faini ya kiasi kisichopungua shilingi laki tatu na kisichozidi Milioni hamsini au kifungo kisichozidi miaka miwili au vyote kwa pamoja, na endapo mtu huyu ni mkosaji wa mara ya pili akitiwa hatiani atawajibika kulipa faini isiyopungua kiasi cha shilingi laki tano na isiyozidi Milioni mia moja au kifungo kisichopungua miaka mitano au vyote kwa pamoja.
“Hii ni kwa mujibu wa Kifungu cha 45 cha Sheria ya Vipimo kama kilivyofanyiwa marekebisho na Kifungu cha 47 cha Sheria ya marekebisho mbalimbali ya Sheria Na. 3 ya mwaka 2016,”amefafanua.
Akizungumzia bei za bidhaa za chakula amesema kuwa ya mahindi kwa mwezi Aprili ni kati ya Shilingi 800 na 1,650 kwa kilo ambapo imepanda kwa asilimia 1.5 ambayo ni sawa na ongezeko la Shilingi 25 kwa kilo, wakati bei ya chini imepungua kwa asilimia 5.9 sawa na punguzo la Shilingi 50 kwa kilo.
Bei ya Unga wa mahindi kwa mwezi Aprili ni kati ya Shilingi 1,200 na 2,100 kwa kilo huku bei ya juu ikishuka kwa asilimia 20.0 sawa na kupungua kwa shilingi 75 kwa kilo, wakati bei ya chini ya unga wa mahindi imeshuka kwa asilimia 20 sawa na kupungua kwa Shilingi 300 ikilinganishwa na bei ya mwezi MaMachi 2023.
Kwaupande wa bei ya mchele kwa mwezi Aprili amesema ni kati ya Shilingi 2,350 na 3,500 kwa kilo huku bei ya juu ya ikishuka kwa asilimia 2.8 sawa na pungufu ya shilingi 100 kwa kilo, wakati bei ya chini ya mchele imeshuka kwa asilimia 13 sawa na pungufu ya shilingi 350 kwa kilo ikilinganishwa na bei ya mwezi Machi 2023
Ametaja Bei ya maharage kwa mwezi Aprili ni kati ya Shilingi 2,175 na 3,800 kwa kilo ambapo bei ya juu ya maharage haijabadilika, wakati bei ya chini imeshuka kwa asilimia 27.2 sawa na pungufu ya shilingi 813 ikilinganishwa na bei ya mwezi Machi 2023.
Pia ametaja na baadhi ya bidhaa zingine za chakula vikiwemo viazi mviringo,unga wa ngano ,sukari pamoja na mafuta yakupikia.
Vilevile ametaja mwenendo wa bei za vifaa vya ujenzi kuwa Bei ya saruji kwa mwezi Aprili ni kati ya Shilingi 14,650 na 24,500 kwa mfuko wa kilo 50, bei ya nondo mm 10 kwa mwezi Aprili ni kati ya Shilingi 16,000 na 23,500 huku bei ya juu ikipanda kwa asilimia 6.8 sawa na shilingi 1,500 ikilinganishwa na bei ya mwezi Machi 2023 ambayo ilikuwa Shilingi 22,000.
Huku bei ya nondo amesema ya mm 12 kwa mwezi Aprili ni kati ya Shilingi 22,000 na 28,000 huku bei ya chini ikipanda kwa asilimia 15.7 sawa na shilingi 3,000 ikilinganishwa na bei ya mwezi Machi 2023 ambayo ilikuwa Shilingi 19,000.
“Bei ya bati nyeupe geji 30 kwa mwezi Aprili ni kati ya Shilingi 21,500 na 30,000. Bei ya juu ya bati imepanda kwa asilimia 9.1 sawa na shilingi 2,500 ikilinganishwa na bei ya mwezi Machi, 2023 ambayo ilikuwa Shilingi 27,500,”amesema.
More Stories
Kapinga atoa maagizo TANESCO ,kuhusu Vijiji vinavyolipia gharama ya mijini kuunganisha umeme
Ukiukaji wa Uhuru wa Kidini na Kutovumiliana Huzusha Malumbano ya Kimataifa
NLD kipo tayari kwa uchaguzi wa Serikali za Mitaa