December 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Vita ya Corona yapamba moto mataifa mbalimbali

Na Mwandishi Wetu

MATAIFA mbalimbali yameendelea kuimarisha hatua za kukabiliana na ugonjwa wa Corona kwa kuoneza siku zaidi ya watu wake kukaa ndani ili kuwakinga na maambukizi.

Hatua hizo zinazidi kuchukuliwa huku kukiwa hakujaonekana matumaini yoyote ya kuweza kutokomeza ugonjwa huo haraka.

UGANDA

Nchini Uganda, Rais wa nchi hiyo, Yoweri Museveni ameongeza siku 21 za wananchi kukaa ndani kuanzia leo hadi Mei 5, 2020 baada ya siku 14 za kwanza kumalizika jana lengo likiwa ni kujikinga na maambuziki ya corona.

Alisema jana kuwa wameongeza siku 21 baada ya kuwepo kwa mafanikio kwa muda wiki tatu tangu kuanza kutangazwa uamuzi hayo.

Rais Museveni alisema suala la usafiri wa umma litajadiliwa na kupendekeza usafiri wa baiskeli kwa sababu unabeba mtu mmoja na ni wa afya.

Alisema kabla ya ugonjwa huo kuingia asilimia 40 ya watu walikuwa wanakufa hospitali kwa sababu ya kula sana na kutofanya mazoezi kwa hiyo baiskeli zitasaidia.

INDIA

Wakati huo huo Waziri Mkuu wa India, Narendra Modi amesema jana kuwa hatua za kuzuia watu kutoka nje nchini humo, ambazo zimewalazimu watu wapatao bilioni 1.3 kubaki majumbani mwao, zitaongezwa muda hadi Mei 3.

Hatua hiyo inakuja licha ya malalamiko kutoka kwa mamilioni ya watu masikini ambao wamebaki bila msaada wowote wakati ajira zimekufa.

Modi alisema kuwa kwa mtazamo wa kiuchumi, India imepata pigo kubwa, lakini maisha ya watu wa India yana thamani kubwa zaidi. Modi alisema inawezekana kulegeza vizuwizi kuanzia Aprili 20.

Hatua za hivi sasa za wiki tatu za kuzuwia watu kutoka nje nchini India zilizowekwa tangu Machi 25 zilitarajiwa kumalizika usiku wa jana India ina kesi 10,000 za maambukizi na vifo 339.

UJERUMANI

Mkuu wa Taasisi ya Afya ya Robert Koch, Lothar Wieler amesema idadi ndogo ya visa vya maambukizi nchini Ujerumani huenda imetokana na upimaji mdogo katika kipindi cha likizo ya Pasaka

Kwa mujibu wa taasisi ya afya ya Robert Koch, ni kuwa huenda visa vichache vya maambukizi ya virusi vya Corona vimetokana na vipimo vichache vilivyofanywa wakati wa likizo ya Pasaka kinyume na inavyodhaniwa kuwa maambukizi hayo yamepungua.

Wieler aliwaambia waandishi wa habari kuwa hawawezi kutoa tathmini ya moja kwa moja kuwa visa vya maambukizi ya virusi vya Corona vinapungua. Aliwataka watu kuendelea kuchukua tahadhari na kufuata maelekezo ya kutokaribiana ili kuzuia kuenea kwa virusi vya Corona.

UINGEREZA

Kwa upande wa Uingereza, idadi ya vifo vinavyotokana na ugonjwa wa COVID-19 iliyoripotiwa huenda ikawa chini tofauti na idadi halisi ya vifo. Kwa mujibu wa takwimu zilizochapishwa jana idadi kamili ya vifo huenda ikazidi asilimia 15 ya ile inayoripotiwa kila siku.

Ofisi ya takwimu za kitaifa alisema kuwa Aprili 3, watu 6,235 walifariki dunia nchini England na Wales kutokana na ugonjwa wa COVID 19, lakini huenda idadi hiyo iliotajwa ikawa chini tofauti na hali ilivyo.

Mtaalamu wa takwimu katika ofisi hiyo, Nick Stripe alisema kuwa idadi ya watu waliokufa kwa ugonjwa wa COVID-19 ni kubwa zaidi ya iliyotajwa kwani ripoti za Serikali zimenakili vifo vilivyotokea hospitali pekee bila ya kujumuisha vifo vilivyotokea majumbani na hata kliniki za kijamii.