*Ikiwa ni hatua ya NIRC kutekeleza ahadi ya Rais Samia
Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online, Dodoma
Tume ya Taifa ya Umwagiliaji(NIRC), imeanza utekelezaji wa ahadi ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya uchimbaji wa visima virefu 67,000 vya maji kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji nchini.
Hatua hiyo Ikiwa ni ahadi ya Rais Dkt.Samia, aliyoitoa wakati wa maazimisho ya siku ya Wakulima Duniani( Nane Nane), yaliyofanyika kitaifa jijini Mbeya, mwaka 2023.

Lengo ni kuhakikisha taifa linaondokana na kilimo cha kutegemea mvua,kuwa na uhakika wa maji yatakayosaidia kulima zaidi ya mara moja kwa mwaka.
Hayo yamesemwa jijini Dodoma na Mkurugenzi Mkuu Tume ya Taifa ya Umwagiliaji (NIRC), Raymond Mndolwa, wakati wa kuanza kwa zoezi la uchimbaji wa visima kwa kutumia mitambo,ilionunuliwa na Serikali katika mashamba ya BBT (Chinangali) ya programu ya “Jenga Kesho iliyo Bora (BBT)”, inayowawezesha vijana kujiajiri katika kilimo.
Mndolwa amesema Serikali imeiwezesha tume kununua mitambo ya kisasa ya kuchimba visima virefu, lengo likiwa ni kuhakikisha kunakuwa na mazingira wezeshi ya upatikanaji wa maji kwa ajili ya kiliimo cha umwagiliaji ambacho kitawezesha kulima mara mbili au zaidi.
“Tume imenunua mitambo 17 ya kuchimba visima kwa thamani ya bilioni 17.5,yenye uwezo wa kuchimba mita 300 hadi 1,800, ambapo mitambo 7 inachimba visima katika shamba la Chinangali na tunashuhudia visima vikiwa na maji ya kutosha,”amesema Mndolwa na kuongeza:
“Miundombinu yote ya umwagiliaji katika shamba hili ipo tayari, na sasa hatua inayofuata ni kuhakikisha maji yanapatikana kwa kuchimba visima 29 hapa na visima vingine 40 vitachimbwa katika shamba la BBT Ndogowe, ili vijana waliopata mashamba haya walime kwa uhakika,”.

Pia amesema,mpango wa uchimbaji visima unatarajiwa kutekelezwa nchi nzima na kuhakikisha kuwa siyo vijana tu, bali wakulima wa kada zote wanapata maji ya uhakika kwa kilimo endelevu.
“Mitambo hii itapita mkoa kwa mkoa, wakulima wajiandae kuchangamkia fursa hii wakiwa katika makundi ya wakulima zaidi ya 16 na ekari kuanzia 40 ili waweze kupata kisima, serikali imedhamiria kumuinua mkulima wa Tanzania, miaka minne iliyopita, miradi ya umwagiliaji ilikuwa 13 pekee, lakini idadi imeongezeka hadi kufikia miradi 780 pamoja na mpango huu wa visima 67,000 nchi nzima,”.

More Stories
Kiongozi wa Mwenge aifagilia RUWASA Tanga
Rais Samia kuanza ziara ya siku saba Simiyu na Mwanza
Msigwa awataka wazazi kuzungumza na watoto wao matumizi mabaya ya mtandao