December 25, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Viongozi,watumishi wa umma wanaojinufaisha kwa rushwa waonywa

Na Daud Magesa,Timesmajira online, Mwanza

VIONGOZI na watumishi wa umma wanaojinufaisha kwa rushwa wametahadharishwa na kutakiwa kuacha tabia hiyo kwa kila mmoja kuwajibika katika nafasi yake na kuwa mstari wa mbele kukemea vitendo vya rushwa kwa maendeleo ya wananchi.

Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Mwanza,James Ruge ametoa rai hiyo Mei 26, mwaka huu wakati akitoa taarifa ya utendaji wa taasisi hiyo katika kipindi cha Januari hadi Machi mwaka huu kwa waandishi wa habari.

Amesema TAKUKURU inatekeleza majukumu yake kwa mujibu wa Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa ya Mwaka 2022 ikishirikiana na wadau wa mapambano dhidi ya rushwa wakiwame watumishi wa umma,taasisi zisizo za kiserikali,mashirika ya umma,vyombo vya habari na vyama vya siasa na wananchi.

“Nawaasa viongozi na watumishi wote wanaotumia nafasi zao kujinufaisha kwa njia ya rushwa kuacha tabia hiyo badala yake wawe mstari wa mbele kuzuia na kukemea vitendo vya rushwa kwa maendeleo ya Watanzania wote,”amesema Ruge.

Amesema katika kuzuia rushwa taasisi hiyo kwa kipindi cha Januari hadi Machi 2023,ilifuatilia miradi 42 ya maendeleo katika sekta zaa afya,elimu na maji yenye thamani ya zaidi ya bilioni 26 kati ya hiyo minne ya thamani ya zaidi ya bilioni 3, ilikutwa na kasoro ambapo ushauri wa kufanya marekebisho ulitolewa.

Ruge amesema mradi wa jengo la wagonjwa wa nje (OPD) la zahanati ya Fumagila linalogharimu zaidi ya milioni 131.5 lilikutwa na kasoro ya mwamko mdogo wa wananchi kuchangia asilimia 10 ya nguvu kazi na fedha.

Pia jengo la wagonjwa wa ndani (IPD) katika zahanati hiyo lenye thamani ya milioni 122.29 kulikuwa na ucheleshwaji wa ununuzi wa vifaa na malipo ya mafundi huku watendaji wa TASAF wakisingizia mfumo wa malipo.

Ambapo msimamizi wa TASAF Jiji alishauriwa kuwasiliana na TAMISEMI ili kurekebisha kasoro za kukatika kwa mfumo wa malipo,kuboresha utendaji wa manunuzi na usimamizi wa vifaa.

Kwa mujibu wa Ruge,walibaini usimamizi duni kwenye ujenzi wa shule ya sekondari mpya ya Buhumbi wilayani Magu, unaogharimu milioni 600,ambao ulikamilishwa chini viwango na vifaa kuharibika ambapo Mratibu wa TASAF na msimamizi wa mradi wameagizwa ukamilishaji huo urudiwe.

“Ujenzi wa .radi wa maji Sagani-Mwamabanza,Magu unaogharimu zaidi ya bilioni 2.5, mitaro ya kulaza mabomba ilichimbwa kwa kina na upana usiokidhi viwango vya mkataba (BOQ).Mhandisi wa Maji na baadhi ya wanakamati walielekezwa mitaro ichimbwe upya,”amesema.

Mkuu huyo wa TAKUKURU amesema wanachunguza malalamiko 81 kati ya 90 ya vitendo vya rushwa yaliyopokelewa katika kipindi cha Januari-Machi, 2023 ambapo Jamhuri ilishinda kesi tatu kati ya nne na kesi mpya nne zilisajiliwa mahakamani na kufanya idadi ya kesi 18 zinazoendelea kusikilizwa.

Pia kipindi cha Aprili hadi Juni mwaka huu, mikakati yao ni kuzuia vitendo vya rushwa kwenye miradi ya maendeleo inayotekelezwa kwa kufanya ukaguzi na kusimamia kwa karibu matumizi ya fedha zinazotolewa na serikali ili kupata thamani ya fedha hizo na dhamira ya serikali kufikisha ustawi bora kwa wananchi.

Aidha wataendelea kutoa elimu ya madhara ya rushwa kwa wananchi kupitia mikutano na vipindi vya redio,kufanya uchambuzi wa mifumo ili kuboresha na kuondoa mianya ya rushwa inayotokana na mifumo ya utendaji.

Pamoja na kuchunguza makosa ya rushwa kwa mujibu wa sheria na kuwachukulia hatua wote watakaobainika kujihusisha na vitendo hivyo.

Ruge amesema katika kuzuia vitendo vya rushwa watashirikiana na wananchi kupitia programu ya TAKUKURU Rafiki kwa wananchi kupata fursa ya kueleza kero zinazowakabili ili zipatiwe ufumbuzi lengo likiwa ni kuboresha utoaji na upatikanaji wa huduma na miradi ya maendeleo kwa kufika ngazi ya kata.

Amewashukuru wananchi kwa ushirikiano unaoifanya kazi ya mapambano dhidi ya rushwa kufanikiwa n hadi sasa kesi 18 zipo mahakama mbalimbali za wilaya mkoani humu na hivyo sote tukishirikiane kuzuia vitendo vya rushwa katika maeneo ya kupata huduma na kwenye miradi ya maendeleo.