January 23, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Viongozi wamfuata Dkt. Salmin Kidombo

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Alhaj Othman Masoud Othman, leo amejumuika na Waumini wa Kiislamu katika Ibada ya Sala ya Ijumaa, huko Mkwajuni Kidombo, Wilaya ya Kaskazini A, Mkoa wa Kaskazini Unguja.

Baada ya Ibada hiyo, iliyohudhuriwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Alhaj Dkt. Hussein Ali Mwinyi, kumefanyika Khitma na Dua Maalum ya kuwaombea Viongozi, Masheikh na Wazee waliopo hai na ambao wameshafariki dunia, ndani na nje ya Kijiji hicho.

Harakati zote hizo ni sehemu ya Mwitikio wa Viongozi, kufuatia Mwaliko wa kila mwaka wa Rais Mstaafu wa Awamu ya Tano ya Zanzibar, Alhaj Dokta Salmin Amour Juma, unaoambatana na Sherehe za Maulid ya Mtume Muhammad (SAW), kiijijini hapo.

Viongozi mbali mbali wa Serikali, Dini, Siasa na Jamii, wakiongozwa na Mufti Mkuu wa Zanzibar, Sheikh Saleh Omar Kaabi, wamehudhuria katika Hafla hiyo.