Na Yusuph Mussa,Timesmajiraonline,Korogwe
MWENYEKITI wa Halmashauri ya Mji Korogwe mkoani Tanga Francis Komba amewaasa viongozi wapya waliochaguliwa kwenye Uchaguzi wa Serikali za Mitaa kuwa maendeleo ya halmashauri na Taifa yanatokana na utendaji mzuri wa uongozi ngazi ya mitaa.
Hivyo, ili halmashauri iweze kukusanya mapato,kuweka mipango ikiwemo uandaaji wa bajeti kwa ajili ya miradi ya maendeleo, itatokana na vikao na mipango kuanzia ngazi ya mtaa.
Aliyasema hayo Novemba 28, 2024 kwenye hafla ya kuapishwa kwa viongozi wa mtaa, ambapo Hakimu Mkazi Mkuu wa Wilaya ya Korogwe Sikitu Mwalusamba, aliongoza zoezi hilo la Uapisho lililofanyika Ukumbi wa Halmashauri ya Mji Korogwe.
“Maendeleo ya nchi yanaanzia kwenu. Utekelezaji wa miradi ya maendeleo unaanzia kwenu na hata mapendekezo ya bajeti ya halmashauri na Serikali kuu yanaanzia kwenu, hivyo ninyi ni watu muhimu kuona nchi inapata maendeleo. Sisi kama halmashauri, tutafuata maamuzi na mapendekezo yenu ili kuona halmashauri inapiga hatua kwenye shughuli za maendeleo” alisema Komba.
Komba alisema dhamana waliyopewa na wananchi ni kubwa, hivyo ni lazima wahakikishe kuwa wanawatumikia wananchi kwa kipindi chote cha miaka mitano, na wao wawe chachu ya kuleta maelewana na kuwaweka wananchi pamoja ili waweze kushiriki shughuli za maendeleo ikiwemo msalagambo bila kuleta msuguano.
“Leo hii niwape hongera kwa kuaminiwa na wapiga kura. Kwa maana hiyo mtakuwa sehemu ya halmashauri, na mtakuwa sehemu ya Serikali, hivyo mnatakiwa kufanya kazi za wananchi wale waliowapa dhamana hiyo kwa kuwasaidia kuondoa changamoto mbalimbali zinazowakabili” alisema Komba.
Msimamizi wa Uchaguzi Halmashauri ya Mji Korogwe Mwashabani Mrope amewataka viongozi wa mtaa kwenda kumsaidia Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kusimamia vema shughuli za maendeleo ikiwemo fedha zinazopelekwa kwenye mitaa yao kwa ajili ya miradi ya maendeleo.
“Tunaowaapisha leo mkiwa mnakwenda kutekeleza majukumu yenu, kubwa mkafanye kazi kumsaidia Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kuona miradi iliyopo ngazi ya mitaa inatekelezwa. Na tukifanya hivyo, tutakuwa tumemsaidia kwa vitendo na sio maneno matupu” alisema Mrope.
Mrope aliisifu timu yake iliyosimamia mchakato huo hadi kukamilika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa hadi kutangazwa matokeo, kwani timu hiyo iliyoundwa na watendaji ngazi ya wilaya, kata na mitaa, ilihakikisha wanafanya kazi usiku na mchana, na wameweza kukamilisha zoezi hilo bila dosari yeyote.
Afisa Uchaguzi wa Halmashauri ya Mji Korogwe Musa Dotti akitoa somo kwa viongozi hao hasa wale waliotoka kwenye vijiji saba na kuwa mitaa kwenye halmashauri hiyo, wameelezwa hawaruhusiwi kukusanya mapato yeyote, kwani kwa muundo wa mitaa, mapato yote yanakusanywa na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Korogwe.
Dotti alisema, pamoja na mambo mengine, wenyeviti wa mitaa wanatakiwa kufuata sheria, kanuni na taratibu katika kuongoza wananchi, na moja ya masharti hayo ni kuhakikisha wanafanya mikutano mikuu ya mtaa kila baada ya miezi mitatu, na Mwenyekiti wa Mtaa ambaye atashindwa kutekeleza mkutano huo kwa mara tatu mfululizo, wananchi wanaweza kumuondoa madarakani.
Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya hafla hiyo ya uapisho, Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Korogwe Mjini Thobias Nungu, alisema wametwaa viti vyote 29 vya wenyeviti wa mtaa, wajumbe mchanganyiko 78, na wajumbe 58 wa kundi maalumu la wanawake, na mafanikio hayo yamekuja kutokana na kujipanga kwa chama hicho.
More Stories
Wahitimu waliosoma MNMA washauriwa kutumia kusanyiko kutoa maoni ya kuendeleza chuo
VETA yaja na mbinu kutatua changamoto sekta ya ukarimu na utalii
Mahakama yashindwa kumtia hatiani Dkt.Nawanda