January 10, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Viongozi wa dini watakiwa kusajili taasisi zao

Na Allan Vicent, TimesMajira Online, Tabora

SERIKALI imewataka Viongozi wa dini kuhakikisha taasisi zao zinasajiliwa ili zitambulike kisheria kutokana na mchango mkubwa wanaotoa katika suala zima la maendeleo ya jamii.

Wito huo umetolewa na Msajili wa Jumuiya za Kiraia kutoka Wizara ya Mambo ya  Ndani ya nchi, Emanuel Kihampa alipokuwa akiongea na Viongozi wa taasisi za dini katika ukumbi wa Mtemi Isike Mwanakiyungi Mjini Tabora jana.  

Alisema mbali na kutoa huduma ya kiroho, taasisi hizo zimekuwa mstari wa mbele kuhamasisha amani na utulivu miongoni mwa jamii hivyo kuchochea juhudi za serikali kudumisha amani na utulivu wa nchi na kuleta maendeleo.

Kihampa alibainisha kuwa serikali imeweka utaratibu mzuri wa kusajili asasi za kiraia ikiwemo jumuiya za kidini ili kutambua mahali zilipo na zinafanya nini katika jamii ili kuzipa ushirikiano unaotakiwa.

Alisisitiza kuwa kila taasisi ya kiraia ikiwemo taasisi za dini ni lazima isajiliwe na iwe na bodi inayosimamia uendeshaji shughuli zake ili kuepusha vitendo vilivyo kinyume na maadili na uvunjifu wa amani miongoni mwa jamii.

‘Serikali inatambua haki na uhuru wa kuabudu kwa wananchi wake, lakini taratibu na sheria ni lazima zizingatiwe kwa kuhakikisha taasisi zote za kiraia zinasajiliwa kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania’, alisema.

Alitaja baadhi ya makundi ya Jumuiya za Kiraia ambayo yanapaswa kusajiliwa ili kutambulika kisheria kuwa ni pamoja na Jumuiya za kidini, Jumuiya za kitamaduni na Jumuiya za Kitaaluma.

Msajili alifafanua kuwa serikali imerahisisha taratibu za usajili wa taasisi hizo ili kuwaondelea usumbufu, hivyo akasisitiza kuwa serikali haitamfumbia macho kiongozi au taasisi yoyote itakayoendelea kufanya kazi bila kusajiliwa.  

Baadhi ya Viongozi wa taasisi za dini waliohudhuria mkutano huo Askofu Peter Shan na Askofu Elias Mbagata walipongeza serikali kwa kurahisisha utaratibu wa kusajili taasisi za dini tofauti na huko nyuma.

Naye Shekhe Ibrahimu Mavumbi aliomba serikali kuweka sheria kali itakayosaidia kudhibiti baadhi ya taasisi zinazokwenda kinyume na maadili ya nchi na kinyume na malengo yaliyobainishwa katika katiba zao.

Msajili wa Jumuiya za Kiraia kutoka Wizara ya Mambo ya  Ndani ya Nchi, Emanuel Kihampa akiongea na Viongozi wa taasisi mbalimbali za kiraia na za dini katika ukumbi wa Mtemi Isike Mwanakiyungi Mjini Tabora jana. Picha na Allan VicentÂ