Na Judith Ferdinand, Mwanza
VIONGOZI wa dini nchini wametajwa kuwa wana wajibu mkubwa wa kutoa elimu kwa jamii ili kufanikiwa mapambano dhidi ya mimba za utotoni na ukatili wa kijinsia kwa watoto wa kike.
Kauli hiyo imetolewa na Askofu wa Kanisa la Africa Inland Church Tanzania (AICT) Dayosisi ya Mwanza, Philipo Mafuja wakati akizungumza na Majira ofisini kwake mkoani hapa.
Amesema maandiko matakatifu ikiwemo Biblia inahitaji viongozi wa dini kuwa sehemu ya kusaidia jamii katika malenzi bora ya watoto.
Kwa msingi huo alisema viongozi wa dini wana mchango na wajibu wa kusaidia Serikali na jamii kwa ujumla katika mapambano ya mimba za utotoni na ukatili ili kuhakikisha watoto wote hususani wa kike wanalindwa hasa katika kipindi hiki cha ugonjwa wa Corona.
Askofu Mafuja, amesema kitu cha msingi katika kipindi hiki ni viongozi wa dini kutoa elimu na kujikita katika kuelimisha wazazi ili waweze kuwalea watoto wao katika malezi bora kwa kufuata maandiko yanavyoelekeza pamoja na kuzingatia maadili ya nchi.
“Viongozi wa dini wanahusika na jamii ambapo kila siku za ibada wanakutana na waumini hivyo wanahusika sana kuisaidia Serikali kwani wanakutana na watu wale wale ambao Serikali inashughulika nao ndio wale wale wanaoingia kwenye nyumba za ibada kazi ya kanisa inatoa huduma za kiroho,” alisema.
Hivyo ameto wito kwa viongozi wa dini kujikita kutoa elimu kwa jamii ambayo itasaidia wazazi na malezi kuwalinda watoto na mimba za utotoni pamoja na ukatili wa aina yoyote.
More Stories
Wassira:Waliopora ardhi za vijiji warudishe kwa wananchi
Rais Samia apongezwa kwa miongozo madhubuti ya ukusanyaji wa kodi
Mwenda:Siku ya shukrani kwa mlipakodi ni maalum kwaajili ya kuwatambua,kuwashukuru