December 27, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Viongozi wa dini watakiwa kuombea Uchaguzi

Na Esther Macha, TimesMajira Online, Mbeya

MKUU wa Mkoa wa Mbeya, Albert Chalamila amesema Taifa litakuwa katika mikono salama endapo viongozi wa dini wataendelea kusimama imara katika kuombea mchakato wa Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 28 mwaka huu umalizike salama kwa kuwachagua viongozi bora.

Chalamila ametoa wito huo wakati akizungumza na viongozi wa dini ambao wametakiwa kuhubiri amani na utulivu katika nyumba zao za ibada kuelekea uchaguzi mkuu na maendeleo katika Mkoa wa Mbeya .

Amesema, kwa sasa jambo kubwa ni kuendelea na maombi ili Taifa liweze kupata kiongozi sahihi atakayeendelea kuhakikisha Tanzania inaendelea kubaki kuwa nchi ya utulivu na amani yenye kupiga hatua za kimaendeleo kwa kasi kubwa.

Pia amewaomba viongozi hao kufunga na kuomba ili kuweza kupata kiongozi sahihi kwani madhara ya kupata kiongozi asiye sahihi aliyeingia bila ya hofu ya Mungu matokeo yake ni kusimama upande wa shetani .

“Ndugu zangu kama hamtapata kiongozi mwenye nguvu ya kukemea basi tujue viongozi wa dini kuna sehemu mlilegea katika majukumu yenu ya kusaidia Taifa kwani misimamo na maonyo yanayotolewa kwenye nyumba za ibada ni muhimu sana kwani kama kondoo watakosa mchungaji (viongozi wa dini) watakuwa wamewaonea kwa sababu hata wakiwa watoto wadogo huonywa,” amesema Chalamila .

Kwa upande wake kiongozi wa kanisa Halisi la Mungu Baba (UWAMBENE) Kuhan Shangwe amesema, wao kama viongozi wa dini wataendelea kuliombea Taifa lakini pia wanatambua kuwa waumini wana akili na wanajua kupambanua mambo mazuri na mabaya.

Shekhe wa Mkoa wa Mbeya, Mohamed Mwansansu amesema, Rais Magufuli lazima aheshimiwe kwani kudharau mamlaka ya nchi ni kuhatarisha amani ya nchi .

“Vitu alivyovifanya Rais Magufuli vinaonekana wazi leo hii unaingia kwenye malumbano ya kutotambua kazi alizofanya hii haipendezi, hebu tumuunge mkono Rais Magufuli ili aweze kutekeleza miradi ya maendeleo” amesema Sheikh Mwansansu.