December 26, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Viongozi wa dini pamoja na vyama vya siasa ,wazee maarufu pamoja na wasimamizi wa uchaguzi ngazi ya jimbo wakiwa katika mkutano wa pamoja na Mkuu Wilaya ya Mbarali ,Ruben Mfune

Viongozi wa dini waombwa kuombea Uchaguzi

Na   Esther Macha, TimesMajira Online, Mbarali

MKUU wa Wilaya ya Mbarali, Reuben Mfune amewaomba  viongozi wa dini wa madhehebu yote  kuendelea kuliombea taifa kama walivyofanya kipindi cha ugonjwa wa Covid-19  ili uchaguzi uweze kufanyika kwa amani .

Mfune ameyasema hayo jana wakati wa kikao cha pamoja kati ya Viongozi wa Dini, Viongozi wa Vyama vya siasa, wazee maarufu pamoja na wasimamizi wa uchaguzi ngazi ya jimbo kwa lengo la kuhamasisha jamii ili iweze kushiriki kikamili uchaguzi Mkuu wa  mwezi October mwaka huu.

Mkuu huyo wa Wilaya amesema kitu kingine walichojadili ni pamoja na maadili kwa vyama vya siasa na wagombea katika kuendesha shughuli za siasa wakati wa kampeni  zikiendelea .

“Wakati tulivyokuwa na changamoto kubwa ya Ugonjwa wa corona mlishiriki kwa kiasi kikubwa kuliombea Taifa letu, msisite kuendelea kuliombea Taifa letu kwa kuwa haya mambo ndiyo yanayoweka mstakabali wa maendeleo ya nchi yetu, tunawaomba katika sala mbalimbali mshirikishe na uchaguzi mkuu ambao ndio utakaotupatia viongozi watakaotuongoza kwa miaka mitano ijayo,”amesema na kuongeza

“Nawasihi sana Vyama vya siasa kufuata ratiba za kampeni kama zilivyopangwa, kufanya kampeni za kistaarabu, kunadi sera na mipango yenu na sio kampeni zenye lugha za matusi, kashfa au kudhalilisha utu wa watu wengine na kwa ambae atakwenda kinyume na taratibu atachukuliwa hatua za kisheria.” Amesema  Mfune

Hata hivyo Mkuu huyo wa Wilaya ameongeza kuwa Uchaguzi ni mchakato unaojumuisha hatua na taratibu mbalimbali za kufuatwa na kuzingatiwa kwani kwani ndio msingi wa uchaguzi kuwa mzuri na wenye ufanisi, kwani itasaidia kupunguza au kuondoa kabisa malalamiko au vurugu wakati wote wa mchakato.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali ambaye ni Msimamizi wa uchaguzi ngazi ya Jimbo , Kivuma Msangi amesema kuwa kwa upande wa jimbo la Mbarali wanachama watano wa vyama tofauti waliochukua fomu za ubunge ila waliorudisha ni wananchama wanne na kwa upande wa madiwani waliochukua fomu ni wanachama 55 wa vyama tofauti na  ambao wamerudisha fomu ni wanachama 54.

Naye Mwanasheria wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali ambaye ni Msimamizi msaidizi ngazi ya jimbo, Jackline Ngaiza ameongeza kuwa, wagombea wote wa nafasi mbalimbali za uongozi pamoja na vyama vyao, wanatakiwa kuheshimu na kufuata Katiba ya Nchi, Sheria ya Uchaguzi, Kanuni za Uchaguzi, maadili ya uchaguzi na maelekezo ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi pamoja na sheria zingine za Nchi katika kipindi chote cha uchaguzi.