December 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

MWENYEKITI wa Kamati ya Kitaifa ya Pamoja ya Maaskofu na Mashekh ya Maadili, Amani na Haki za Binadamu kwa Jamii ya Madhehebu ya Dini zote nchini, Askofu William Mwamalanga,

Viongozi wa dini wajitosa sakata la sukari

Na Mwandishi Wetu

MWENYEKITI wa Kamati ya Kitaifa ya Pamoja ya Maaskofu na Mashekh ya Maadili, Amani na Haki za Binadamu kwa Jamii ya Madhehebu ya Dini zote nchini, Askofu William Mwamalanga, amewataka wafanyabiashara wa bidhaa ya sukari kuacha mara moja kuficha bidhaa hiyo na badala yake kuwauzia wananchi kwa bei sitahiki  inayolinda mtaji wao.

Askofu Mwamalanga ametoa kauli kupitia taarifa yake kwa vyombo vya habari jana akisema ameshuhudia baadhi ya Waislamu jijini Dar es Salaam wakifuturu futali isiyo na sukuri.

Alishauri Serikali kukaa meza moja na wafanyabiashara kuangalia namna ya kulitafutia ufumbuzi suala la bei ya sukari, kwani katika maeneo mengine inauzwa hadhi sh. 4,500 hadi sh.5,000.

Amesema endapo wadau hao watakaa meza moja watotoka na lugha moja itakayowasaidia wananchi kote nchini. Amesema hakuna sababu ya watendaji wa Serikali kuwakamata wafanyabiashara kwani hiyo siyo njia sahihi ya kuwasaidia Watanzania.

Askofu Mwamalanga amesema dawa ya upungufu wa sukari ni biashara hiyo kubaki kwenye soko huru la ushindani na kwamba hapo itajipunguza yenyewe kama zilivyo nguo. Alisema tatizo hilo linaweza kuwa linachangiwa na ukiritimba wa kutoa vibali vya kuagiza sukari.

Amevitaka viwanda vya ndani kuzalisha sana sukari na kuweka akiba ya kutosha ili wanapoingia kwenye hatua ya kufunga viwanda kwa matengenezo taifa liwe na sukari ya kutosha kwa matumizi ya ndani ikiwa ni pamoja na kuacha kuuza nje wakati ndani hatuna bidhaa hiyo.

“Hauwezi kulinda viwanda vya ndani visivyozalisha. Wimbo huu ni wa miaka yote tukizalisha zaidi hatutakuwa na haja ya kuagiza nje,” alisema na kutahadharisha kwamba tatizo la sukari linaweza kuichonganisha Serikali ya awamu ya Tano na wananchi wake bila sababu za msingi,” amesema Askofu Mwamalanga.

Aidha Askofu Mwamalanga amewataka wafanyabiashara kote nchini kuacha kuficha sukari kwani kufanya hivyo ni dhambi mbele za Mungu.

“Sukari ni chakula unapoficha chakula unagombana na Mungu, wahurumieni Watanzania wenzenu mtabarikiwa zaidi ya hapo mlipo,”amesema.