March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Viongozi wa dini wahimizwa kukemea maovu,kulinda umoja wa taifa

Na Mwandishi wetu, Timesmajira Online 

VIONGOZI wa dini nchini wamehimizwa kuwa mstari wa mbele kukemea maovu katika jamii huku wakisimamia maridhiano, kulinda maadili ya Kitanzania na kudumisha umoja wa waumini bila kujihusisha na siasa.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar-es-Salaam,Desemba 30,2025 Mwalimu Katekesi wa Kanisa Katoliki Dodoma, Joseph Ludovick,amesema viongozi wa dini wana jukumu la msingi la kusimamia haki na wajibu wa jamii kwa kukemea mienendo inayopotosha maadili pindi inapojitokeza.

Amesema  kuwa kanisa si chama cha siasa, bali ni taasisi iliyowekwa na Mungu kuwatumikia watu kwa kutangaza Injili, kuhimiza maadili mema na kulinda misingi ya haki, amani na upendo miongoni mwa waumini.

“Kuingiza siasa za vyama ndani ya taasisi za kidini kunaweza kuleta mgawanyiko usio wa lazima miongoni mwa waumini, jambo linaloweza kudhoofisha dhamira ya kanisa ya kuwaunganisha watu na kuwalea kiroho na kimaadili,”amesema.

Pia amesema,kanisa halipaswi kufungamana na upande wowote wa kisiasa kwa lengo la kuwavutia au kuwaelekeza waumini wake kisiasa, bali libaki kuwa msimamizi wa maadili na sauti ya dhamira inayokemea uovu bila upendeleo.

Sanjari  na hayo amewahimiza viongozi wa dini kutumia nafasi zao kutoa mwanga wa kimaadili na kijamii katika masuala ya taifa, kwa kushauri kwa hekima na kusisitiza maridhiano, badala ya kuchochea misimamo inayoweza kuvuruga amani.