May 9, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Viongozi wa Dini waaswa kuimarisha mafundisho kwa wanandoa kunusuru kuvunjika kwa ndoa

Na Joyce Kasiki,Timesmajira online,Dodoma

WAZIRI wa Maendeleo ya Jamii Dkt.Dorothy Gwajima amewaasa viongozi wa Dini zote nchini kuimarisha mafundisho kwa wanandoa kabla na baada ya kuingia kwenye ndoa ili kuwanusuru na mifarakano inayopelekea ongezeko la kuvunjika kwa ndoa na hivyo kusababisha watoto kukosa malezi bora na hivyo kuathiri ukuaji wao..

Dkt Gwajima ameyasema hayo leo Mei 8,2025 wakatin akizungumza na waandishi wa habari kuhusu siku ya familia inayofanyika Mei 15 ya kila mwaka ambapo mwaka huu yanatarajiwa kufanyika mkoani Mwanza .

 “Ndugu zangu kila siku tunashuhudia harusi ,michango ya harusi,sisi wote kama jamii tunapaswa tukae tutengeneze kama tunavyotengenezaga harusi zetu kuwa nzuri,tujadili na tuwe na mafundisho katika jamii yanayomuandaa mtoto wa kiume na mtoto wa kike kwamba unapokwenda kwenye ndoa utarajie nini,na ufanye nini,

“Vikombe viwili vikikaa pamoja havikosi kugongana siku moja ,je unavisogezaje ili kila kimoja kiwe na nafasi virudi tena kabatini,hii ndiyo mijadala tunayotakiwa tuifanye na kuifanikisha kama jamii ,na kama tunavyofanya mijadala mingine ,lengo ni kuondoa kuvunjika kwa ndoa.”amesema Dkt.Gwajima

Amesema,Wizara yake kwa kushirikiana na viongozi wa dini, imeandaa vitabu vya malezi ya watoto kwa muktadha wa dini ya kikristo na kiislam vinavyojulikana kwa jina la wazazi wangu kesho yangu ili kuwaelimisha waumini wa dini hizo namna ya kulea watoto wakiwa na hofu ya Mungu.

Aidha amesema ,Serikali itaongeza  wigo wa upatikanaji wa vitabu hivyo na niwaombe wananchi kufuatilia taarifa  zinazowekwa kwenye kurasa za wizara mbalimbali ili kupata taarifa muhimu zikiwemo za malezi ya watoto.