November 27, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Viongozi wa dini Katavi waomba wananchi kujitokeza kupiga kura

Na George Mwigulu,Timesmajiraonline, Katavi.

SHEKHE Mkuu wa Mkoa wa Katavi Mashaka Kakulukulu,amesema kuwa wananchi Mkoa wa Katavi wanapaswa kutambua wanahaki mbalimbali zinazotambuliwa na sheria ikiwamo kupiga kura kesho Novemba 27, 2024 kumchagua kiongozi wamtakaye kwa maendeleo yao.

Mbali na kupiga kura wanapaswa kutambua wanahaki na wajibu wa kuheshimu maamuzi yawengine kwa ajili ya kudumisha amani na usalama wa jamii.

Shekhe Mkuu wa Mkoa wa Katavi Mashaka Kakulukulu, akihutubia Jumuiya ya Maridhiano na Kamati ya Amani inayoshirikiana na dini mbalimbali katika ukumbi wa Mpanda Social Hall Manispaa ya Mpanda Mkoa wa Katavi amesisitiza wananchi kujitokeza kwa wingi kupiga kura.

Kiongozi huyo wa kidini, Amesema viongozi wa serikali za mitaa watakao chaguliwa ni muhimu kwa kuwa watakwenda moja kwa moja kushughurika na jamii kwa ngazi ya chini zaidi na jambo linalovutia serikali imeweka mazingira mazuri ya usalama na amani yatakayo mwezesha mwananchi kupiga kura.

“Tunashukuru mazingira yamewekwa vizuri na hali ya utulivu ipo, Hali ya amani ipo  hivyo naendelea kuwasihi  amani tuliyo nayo tuendelee kuwa nayo na uvumilivu tulionao tuendelee nao na tuvumiliane hadi pale uchaguzi utakapo kwisha” Amesema Shekh Kakulukulu.

Richard Frances, Askofu wa Jimbo la Katavi wa Kanisa la Gosple Revival Assemblies of God amewaasa waumini wa dini mbalimbali kukataa vishawishi vya watu wenye nia mbaya ya kuwalaghai wasipige kura.

Amesema wananchi wanapaswa kufahamu kuwa serikali imetoa fursa ya siku moja pekee ya kujitokeza kwa wingi kwenda kupiga kura kwa ajili ya kuwachagua viongozi wao.

“Muumini unayemtegemea Mwenyezi Mungu umeshawishika kwa kupewa fedha kidogo ambayo itakufanya upate shida ya hukumu ndani ya dhamiri yako kwa sababu ya kupewa rushwa na mgombea, Tambua rushwa ni adui wa haki na hupotosha haki hivyo fanya maamuzi sahihi ya kupiga kura isiyo na ushawishi wa fedha” Amesema Askofu huyo.

Jeniffer Mlay Mkazi wa Manispaa ya Mpanda Mkoa wa Katavi amesema kuwa amejiandaa kupiga kura ya kuchagua viongozi kwani wakati wa kampeni ameweza kupata fursa ya kusikiliza sera za wagombea mbalimbali ambapo tayari ameshaona ni mgombea yupi atakaye kwenda kumpigia kura kesho Novemba 27, 2024

Vilevile amewaomba wananchi wote hususani wanawake na vijana kutokubaki nyuma bali wawe masitali wa mbele kwenda kupiga kura.

Uchaguzi wa serikali za mitaa ni miongoni mwa muhimu muhimu wa demokrasia inayowezesha ushiriki wa wananchi katika uongozi wa viongozi wa maeneo yao. Uchaguzi huo unatoa nafasi kwa wananchi kuwachagua viongozi wanaowaamini li kuleta maendeleo na kuboesha huduma za kijamii ngazi za mitaaa.