December 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Viongozi wa CCM watakiwa kushiriki vikao vya mashina

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online, Shinyanga

KATIBU Mkuu wa Chama cha Mapinduzi Ccm,Daniel Chongolo amewataka Viongozi ngazi zote nchini kuanzia Tawi, Kata, Wilaya Mkoa na Taifa kuhakikisha wanashiriki vikao vya mashina Ili kuendelea kukiimarisha Chama hicho kwani msingi wa uimara wa CCM ni ngazi hizo.

Amesema ngazi zote za Viongozi, kuanzia tawi, Kata, Wilaya, Mkoa na Taifa tushuke chini kushiriki vikao vya balozi ngazi za mashina, kwani mshina ndio uimara wa Chama chao Cha Mapinduzi.

Chongolo ameyasema hayo Jana mkoani Shinyanga shina namba 6 Wilayani Kishapu katika Ziara yake inayoendelea ikiwa na na lengo la kukagua na kuhamasisha uhai wa Chama pamoja na kukagua utekelezaji wa Miradi ya Maendeleo.

Amesema kutokana na changamoto za baadhi ya miradi kuchelewa kukamilika kwa uhaba wa fedha, Katibu Mkuu wa CCM, Daniel Chongolo amezielekeza halmashauri kuacha kugawanya fedha katika miradi mingi na hivyo kushindwa kuikamilisha.

Katika maelekezo yake wakati akikagua mradi wa daraja la Ipeja-Itilima wilayani Kishapu, Chongolo alisema ni vema kwa halmashauri kuelekeza fedha katika miradi michache itakayokamilika.

“Sio mnapewa bilioni moja mnapeleka kwenye miradi 40, ambayo haikamiliki, hizo zama zimepita tunataka fedha zielekezwe kwenye mradi unaokwenda kukamilika kwa asilimia 100,”amesema na kuongeza

“Na sio fedha zitolewe kidogo kidogo zikafanye kazi kidogokidogo tija yake haionekani, hayo ndiyo mambo tunayotaka,”amesema

Hata hivyo, amepongeza hatua ya kukamilika kwa mradi wa daraja hilo, lililogharimu Sh486.4 milioni badala ya Sh500milioni zilizotengwa.

Katika hatua nyingine, Chongolo amehaidi kushinikiza upatikanaji wa fedha kutoka mfuko wa dharura kugharimia ujenzi wa mradi wa barabara ya Kolandoto-Meatu yenye urefu wa kilometa 53.