- Uwanja wa Uhuru waelemewa, mamia wapoteza fahamu wakiaga mwili wa Hayati Dkt.Magufuli, marais 11, wawakilishi wa mataifa 50 kutoa heshima kitaifa Dodoma leo, wananchi wasimulia alivyobadilisha heshima ya Tanzania muda mfupi
Penina Malundo na Joyce Kasiki, TimesMajira Online, Dar es Salaam na Dodoma
MAELFU ya Watanzania wamejitokeza kwa siku ya pili katika Uwanja wa Uhuru uliopo Halmashauri ya Manispaa ya Temeke mkoani Dar es Salaam kuuaga mwili wa aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Hayati Dkt.John Magufuli ambaye alifariki Machi 17, mwaka huu katika Hospitali ya Mzena iliyopo mkoani humo wakati akipatiwa matibabu ya ugonjwa wa mfumo wa umeme.
Shughuli ya kuaga mwili wa Hayati Rais Magufuli ilianza asubuhi majira ya saa moja ambapo wananchi walioanza kufurika tangu saa 12 asubuhi walipata fursa ya kuanza kuaga mwili huo kwa kupita katika chumba maalum kilichokuwa uwanjani hapo kilichoweka mwili kwa ajili ya kuaga.
Aidha, kutokana na idadi hiyo kuwa kubwa, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene aliagiza Jeshi la Polisi kusimamia vema watu kuingia na kutoka nje ya uwanja huo ili watu wote wapate nafasi ya kutoa heshima ya mwisho kwa mpendwa wao.
Wakati wa zoezi hilo la kuuaga mwili huo, maelfu walifurika katika uwanja huo ambao una uwezo wa kuchukua watu zaidi ya watu 60,000 huku wengine wakikosa nafasi na kulazimika kusubiria nje.
Majira lilishuhudia simamzi, vilio huku wananchi wengine wakizirai na kupoteza fahamu ndani ya uwanja huo ambapo vyombo vya ulinzi na usalama vilishirikiana bega kwa bega na wananchi wengine kutoa huduma za haraka kwa kila mmoja.
Kutokana na wingi huo wa watu, Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Godwin Gondwe alilazimika kutoa muongozo mara kwa mara kwa wananchi ili kuhakikisha kila mmoja anamuaga Hayati Dkt.Magufuli.
“Ndugu wananchi wote wa Dar es Salaam, tunawashukuru wote kwa kuja kwa ajili ya kumuaga mpendwa wetu na kutoa heshima, tunawahakikishia wote mtapata nafasi, lakini kwa idadi ya watu walioko hapa naomba walioko majukwaani wasinyanyuke hadi watakaporuhusiwa, walioko nje wasiingie wabakie huko hadi wa ndani wapungue, ” alisema DC Gondwe.
Baada ya kuonekana watu ni wengi utaratibu wa kuaga ulibadilishwa na mwili wa Hayati Magufuli kupitishwa uwanja mzima ili kutoa fursa ya watu wote kuaga kwa kupunga mikono.
Mkuu wa Wilaya ya Temeke Godwin Gondwe alitangaza zoezi hilo na kuwaambia watu kuupungia mkono mwili huo pindi unapozungushwa katika viwanja hivyo.
Mwili huo uliweza kuzungushwa mara tano katika viwanja hivyo ili kuwapa nafasi wananchi wa Dar es Salaam kutoa heshima zao za mwisho.
Aidha,kufuatia watu kuanguka na wengine kupoteza fahamu baada ya kutoa heshima zao za mwisho kwa mwili wa Hayati Dkt. Magufuli watoa huduma ya usaidizi walilazimika kuwa na kazi ya mara kwa mara ya kuwabeba na kuwaondoa wanaoanguka ili kuwezesha wengine nao kupata nafasi ya kuaga mwili huo.
Msafara uliobeba mwili wa Hayati Dkt.Magufuli uliondoka jana jioni kuelekea jijini Dodoma kwa ajili ya wananchi wa mkoa huo kupata nafasi ya kuuaga leo kabla ya kuelekea Zanzibar kesho, baadaye Mwanza na kumalizia Chato mkoani Geita ambako atapumzishwa kwenye nyumba yake ya milele Machi 26, 2021.
Wakati huo huo Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari,Utamaduni,Sanaa na Michezo, Dkt.Hassan Abbas amesema,viongozi mbalimbali wa kitaifa na kimataifa wanatarajiwa kuhudhuria kwenye mazishi ya Kitaifa ya aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.John Magufuli yanayofanyika leo mkoani Dodoma.
Akizungumza na waandishi wa habari katika viwanja vya Jamhuri ambapo shughuli hiyo ya mazishi itafanyika,Dkt. Abbas alisema, viongozi hao watapata fursa ya kuaga mwili wa Dkt.Magufuli na baada ya hapo wananchi pia watapata fursa hiyo.
ìMsiba huu siyo tu umeigusa Tanzania bali umeigusa Dunia,hivyo viongozi mbalimbali wa Kimataifa nao wataungana nasi kumuaga Dkt.Magufuli wakiwemo marais na wawakilishi 11 mpaka sasa wameshathibitisha kushiriki,îalisema Dkt.Abbas
.
Pia alisema, zipo Jumuiya za Kimataifa,mabalozi,asasi za kikanda zaidi ya 50 pia zitashiriki.
Aidha, alisema watakaoshiriki ni Rais wa Kenya, Rais wa Malawi, Rais wa Comoro, Rais wa Msumbiji, Rais wa Zimbabwe, Rais wa Zambia, Rais wa Namibia, Rais wa Botswana, Rais wa Afrika Kusini na Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo huku akisema marais wa nchi za Rwanda,Burundi na Angola watawakilishwa.
Dkt.Abbas ambaye pia ni Msemaji wa Serikali alisema, mwili wa Dkt.Magufuli utaanzia Bungeni ili wabunge wapate fursa ya kutoa heshima za mwisho na baadaye utapelekwa katika viwanja vya Jamhuri.
Wananchi wamzungumzia Dkt.Magufuli
Dkt.Abbas aliwataka wananchi wa Mkoa wa Dodoma kujitokeza kwa wingi katika shughuli hiyo ya mazishi ya Kitaifa kuanzia saa moja asubuhi.
Baadhi ya wananchi waliojitokeza katika viwanja vya Nyerere jijini Dodoma kusaini kitabu cha maombolezo walimzungumzia kiongozi huyo huku wakisema watamkumbuka kwa mengi aliyoyafanya katika mkoa huo.
Kuruthumu Iddy Mjumbe wa CCM Kata ya viwandani Mtaa wa Kinyali alisema kuwa, pengo la Rais Magufuli ni kubwa sana hasa kwa watanzania wanyonge na masikini kwani yeye alikuwa kimbilio la watanzania wa hali ya chini.
“Rais Magufuli alikuwa kimbilio la wanyonge napata wakati mgumu sana kumuelezea namuombea sana kwa Mungu apumzike kwa amani kwani tuko katika wakati mgumu sana hasa katika kipindi hiki tulipompoteza kiongozi wetu mpendwa,”alisema Kuruthumu na kuongeza kuwa
,”Tena kwa sisi wana Dodoma ametufanyia mambo mengi ambayo yameibadilisha Dodoma,ametuletea makao makuu,amepanua uwanja wa ndege wa Msalato,ametujengea soko kubwa la Ndugai ambalo wajasiriamali wadogo pia tutapata vizimba,kwa kweli tutamkubuka Rais wetu,” alisema.
Alisema, CCM kimeondokewa na Mwenyekiti huyo wa taifa na kuacha pengo kubwa ndani ya chama,pia alisema ni wakati wa kumuombea Rais Mama Samia Suluhu Hassan kuyaendeleza yale mema yaliyoachwa na Hayati Magufuli.
Mzee Michael Ayoub mkazi wa Dodoma alisema, amepokea kwa masikitiko makubwa kifo cha Magufuli kwani aliwapa kipaumbele wazee kwa kuhakikisha wanapatiwa matibabu.
“Nakosa maneno mengi ya kumzungumzia mpendwa wetu sisi wazee alitupenda sana alitujali na kutupa kipaumbele wazee tumekuwa tukiheshimika na kulindwa,naumia sana sana mpaka nakosa ya kusema kikubwa tumuombee sana kwa Mungu,”alisema Mzee Ayub.
Kwa upande wake Jasmini Ibrahimu mwanafunzi wa Shule ya Sekondari Dodoma alisema, kama mwanafunzi alikuwa anafuatilia jinsi Rais Magufuli alivokuwa akifanya kazi Magufuli kusaidia sana katika elimu na kuhakikisha wanafunzi wanasoma katika mazingira mazuri ikiwemo kuboreshewa miundombinu.
“Katika uongozi wake tumepata elimu bure imesaidia wazazi hata ambao hawakua na uwezo wa kutusomesha tumeweza kusoma tumeumia sana kama wanafunzi hakika tumepoteza kiongozi shujaa katika nchi yetu,”alisema mwanafunzi huyo.
More Stories
Watoto wenye uhitaji wapatiwa vifaa vya shule
Wananchi Kisondela waishukuru serikali ujenzi shule ya ufundi ya Amali
RC.Makongoro ataka miradi itekelezwe kwa viwango