December 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Vikundi vya wafugaji nyuki vyawezeshwa

Na Esther Macha, TimesMajira Online, Songwe

VIKUNDI vitano vya wafugaji wa nyuki katika Halmashauri ya Wilaya ya Songwe vimewezeshwa mtaji na vifaa ili viweze kujitegemea na kuondokana na umasikini.

Vikundi hivyo vimewezeshwa na kampuni ya uchimbaji wa madini ya Shanta Gold Mine (New Luika) ikiwa ni sehemu ya mchango wake kwa jamii.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo Kwa vikundi hivyo, Kaimu Meneja wa Shanta Gold Mine (New Luika) Exupery Lyimo amesema kampuni hiyo imeviwezesha vikundi hivyo kutoka maeneo ya Saza na Mbangala.

Amesema, kampuni hiyo ilianza kuviwezesha vikundi hivyo mwaka 2017 Kwa kuanza kuvipa mizinga ya nyuki na kwamba kampuni yenyewe ndio mnunuaji wa asali ambazo zinazalishwa na vikundi hivyo.

Baada ya kunzisha vikundi hivyo kampuni ya Shanta ilitoa Jumla ya Mizinga 250 Kwa vikundi hivyo katika maeneo ya Saza na Mbangala pamoja na mashine 10 zinazotumika kuvuna asali.

“Mheshimiwa DC, alitufuata kama wadau wa maendeleo katika wilaya yetu ya Songwe ili pamoja na mambo mengine tuone ni Kwa namna gani tunashurikiana na jamii katika eneo la ufugaji nyuki, pamoja na kutoa Mizinga hiyo, pia tuliwaleta wataalamu wa nyuki kutoka Tabora Kwa ajili ya kutoa elimu,” amesema.

Kwa upande wake mkuu wa wilaya ya Songwe, Samwel Jeremiah amezitaka taasisi za kifedha wilayani humo kupunguza masharti ya kukopa ili vikundi hivyo vikufaike na mikopo bila kuumia.

“Ufugaji wa nyuki ni fursa sio dhahabu Tu hata huku kwenye nyuki unaweza ukawa tajiri ukajiingizia kipato cha kutosha,” amesema Jeremiah.

Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Songwe, Francisca Nzota amesema, Kati ya vikundi hivyo, ni vikundi viwili peke yake ndivyo vilifaidika na mkopo wa halmashauri katika mwaka wa fedha 2018/19.

Amesema, vingine havijanifaika Kwa sababu havijakidhi masharti ingawa halmashauri inaendelea kutoa elimu ili navyo viweze kupata mkopo.

Katibu wa kikundi cha nyuki Group, Edward Charles amesema, walinza na Mizinga 15 lakini baadae kampuni ya Shanta iliwaongezea mizinga 100 na kwamba baada ya kurina asali wanaiuzia kampuni ya Shanta.

Lita moja ya asali wanauza sh.10,000, huku akieleza kuwa tangu waanze kufuga nyuki maisha Yao yamebadilika kutokana na kuwa na uhakika wa kupata kipato.