Na Mwandishi wetu, Timesmajira Online, Mbeya
VIKUNDI vya ngoma za asili nchini vimetakiwa kujisajili katika Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA), ili kupata utambulisho rasmi na vibali vinavyowawezesha kushiriki katika maonesho na shughuli mbalimbali za sanaa kwa mujibu wa taratibu.
Hayo yamesemwa na mwakilishi wa Wizara ya Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo,Daniel Chilonzi wakati wa maadhimisho ya miaka kumi ya Taasisi ya Tulia Trust, yanayokwenda sambamba na Tamasha la Ngoma za Asili lililofanyika katika Mtaa wa Gombe, Kata ya Itezi jijini Mbeya.
Amesema Serikali inatambua mchango wa matamasha ya ngoma za asili katika kuhifadhi na kuendeleza utamaduni wa Tanzania, lakini amesisitiza umuhimu wa vikundi hivyo kufuata taratibu za usajili.
“Tunavitaka vikundi vya ngoma za asili kujisajili BASATA, kwa sababu usajili unaviwezesha kutambulika rasmi na kupata vibali vya kushiriki katika maonesho na shughuli mbalimbali za sanaa kwa mujibu wa taratibu,” amesema mwakilishi huyo.
Kwa upande wake, Afisa Habari wa Taasisi ya Tulia Trust, Joshua Mwakanolo, amesema ngoma za asili ni miongoni mwa nguzo muhimu za utamaduni wa Tanzania na zinapaswa kupewa nafasi ya kuendelezwa.
Mwakanolo amesema kupitia matamasha ya ngoma za asili, wasanii wanapata fursa ya kuonesha vipaji vyao, kujitangaza na kupata nafasi ya kushiriki katika matukio mbalimbali.
Amesema mwitikio mkubwa wa vikundi vinavyoshiriki katika tamasha hilo unaonesha namna sanaa ya ngoma za asili ilivyo na mvuto kwa jamii.
Ameongeza kuwa zaidi ya vikundi 120 vya ngoma za asili vimehudhuria na kushiriki katika tamasha hilo, hali anayoeleza kuwa ni ishara kwamba utamaduni unaweza kuwa fursa ya kuwaunganisha vijana, kukuza vipaji na kuchochea shughuli za kiuchumi.




More Stories
NHIF, Aga Khan kuimarisha huduma za saratani Nchini
EWURA yatoa elimu Nishati, Maji maonyesho Geita
VETA yatambulisha mavazi salama migodini