September 26, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

BoT yanunua Tani 34 za Dhahabu kuongeza akiba



Na Joyce Kasiki, Geita


BENKI Kuu ya Tanzania (BoT) imenunua takriban tani 34 za dhahabu kutoka kwa wachimbaji wadogo, wa kati na wakubwa walio rasmi, hatua iliyosaidia kuongeza akiba ya fedha za kigeni nchini kwa takriban dola za Marekani bilioni 2.05.


Akizungumza Sept 25,2026 kuhusu mpango huo kwenye maonyesho ya Teknolojia ya Madini mkoani Geita kwenye viwanja vya Dkt.Samia Suluhu Hassan ,Mchambuzi wa Fedha Mwandamizi kutoka BoT, Idara ya Masoko ya Fedha za Nje, Glory Gabriel Maembe, amesema mpango wa ununuzi wa dhahabu umeendeshwa kwa takriban miaka miwili na umekuwa na mchango katika kuongeza akiba ya Taifa.


Amesema mpango huo pia umewezesha kuwepo kwa soko la uhakika kwa wachimbaji wa dhahabu, huku ukichangia urasimishaji wa shughuli za uchimbaji na biashara ya madini nchini.


Kwa mujibu wa Maembe, mpango huo umeendelea kuunga mkono ukuaji wa viwanda vya ndani vya kusafisha dhahabu, maarufu kama local refineries, hatua inayolenga kuongeza thamani ya dhahabu kabla ya kuuzwa katika masoko ya nje.


Aidha, amesema wachimbaji wameendelea kunufaika na unafuu wa baadhi ya tozo, ikiwamo kupunguzwa kwa kiwango cha mrabaha kutoka asilimia sita hadi nne, kufutwa kwa ada ya ukaguzi ya asilimia moja na kuondolewa kwa kodi ya ongezeko la thamani (VAT).


Ameongeza kuwa malipo kwa wachimbaji yanafanyika kwa haraka, ambapo utaratibu uliowekwa unalenga kuhakikisha malipo yanakamilishwa ndani ya saa 24.


“Mpango huo wa BoT unalenga kutumia dhahabu inayozalishwa nchini kama sehemu ya juhudi za kuongeza akiba ya fedha za kigeni, sambamba na kuimarisha mnyororo wa thamani katika sekta ya madini.”amesisitiza Maembe