November 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Sura iliyoathiriwa na vipodozi vyenye viambato vya sumu

Vijue vipodozi vyenye vyambato vya sumu, madhara yake kiafya

Na Penina Malundo

KIPODOZI ni kitu chochote ambacho kinatumika katika kupaka,kupulizia au kujifukiza katika mwili wa Binadamu kwa lengo la kusafisha ,kuboresha muonekano na kumfanya mtu awe tofauti na hali yake ya kawaida.

Shirika la Viwango nchini (TBS)ni shirika lenye dhamana ya kusimamia ubora na usalama wa vipodozi vinavyoingia kutoka nje ya nchi na vinavyozalishwa nchini.

Zipo malighafili nyingi zinazotumika kutengenezea vipodozi lakini vipo viambata ambavyo haviruhusiwi kutumika katika uzalishaji wa vipodozi hivyo.

Viambata hivyo vimekuwa vikitumika katika kuchanganywa kwenye vipodozi ikiwemo mafuta ya kupaka mwili hali inayobadilisha rangi ya mwili.

TBS imekuwa ikifanya kazi kubwa ya kuhakikisha vipodozi ambavyo vinaviambata vyenye sumu haviruhusiwi kuingia nchini kwa lengo la kuhakikisha inalinda afya za watumiaji.

Vipodozi vingi vinavyotumika kupakwa kwenye ngozi ya binadamu kwa kiasi kikubwa vinasababisha madhara katika mwili na wakati mwingine kusababisha hata saratani .

Vipo viambata vingi vinavyochanganywa katika vipodozi,ambapo vingine tayari vimepigwa marufuku kama ikiwemo Hydroquinone,Halogenateda Salicylanilide,Zirconium,Steroids na Zebaki.

Kutokana na juhudi zinazofanywa na Shirika la TBS,kuendelea kutoa elimu mara kwa mara kwa watumiaji wa vipodozi na wauzaji wa vipodozi imekuwa ikisaidia vipodozi vingi ambavyo havikidhi viwango kutoingia sokoni.

Pia shirika hilo limekuwa likishiriki katika mikusanyiko mbalimbali kwa lengo la kutoa elimu katika maonyesho ya sabasaba,Nanenane na pia kuwepo kwa programu mbalimbali za kupita katika Shule ,Vyuo kwa lengo la kutoa elimu juu ya matumizi ya vipodozi.

Utoaji wa elimu juu ya matumizi sahihi ya vipodozi kwa kiasi kikubwa yanaokoa maisha ya kesho kwa watoto na kujua ni namna gani vipodozi vinamadhara hususani vyenye viambata vya sumu.

TBS imekuwa mstari wa mbele kuwatembelea na kufanya kaguzi wauzaji na wasambazaji wa biashara ya vipodozi hususani kuwaelimisha matumizi sahihi ya vipodozi.

Mara nyingi wafanyabiashara hao wanaouza vipodozi ushauriwa kuuza vipodozi ambavyo vina alama ya TBS na uwapa orodha ya vipodozi vyenye viambata vya sumu.

Ni jukumu la kusimamia ubora, usalama na ufanisi wa dawa, vipodozi na vifaa tiba kwa kufanya tathmini na usajili, ukaguzi, ufuatiliaji wa ubora na usalama wa bidhaa hizo kwenye soko, usajili wa maeneo ya biashara ya bidhaa mbalimbali ikiwemo vipodozi.

Tafiti mbali mbali zimebainisha kuwa kuna zaidi ya asilimia 52 ya wanawake hutumia Vipodozi mbali mbali vyenye viambatishi vyenye sumu ambavyo vinaweza kusababishia matatizo katika afya ya binadamu.

Miongoni mwa magonjwa yanayoweza kutokea baada ya kutumia vipodozi vyenye viambatana sumu ni pamoja na ugonjwa wa kansa ya ngozi, figo pamoja na kutoshika ama kuharibika kwa mimba kwa mama mjamzito.

Madhara ya vipodozi kwenye mikono

Takwimu zilizokusanywa na Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) mwaka 2011 zilionesha kwamba asilimia 40 ya wanawake Waafrika hupausha ngozi zao.

Katika mataifa mengine idadi hiyo ni ya juu na ufikia hadi Asilimia 77 ya wanawake vipodozi hivyo kwa nchi ya Nijeria, Togo ikiwa asilimia 59, Afrika ya Kusini ikiwa asilimia 35, Senegali ikiwa asilimia 27 huku Mali ikiwa asilimia 25 wanatumia bidhaa za kupausha ngozi.

Matumizi ya muda mrefu ya vipodozi vyenye viambata vya sumu husababisha utegemezi au uraibu kwani ngozi hurejelea rangi ya asili matumizi yakisitishwa kwa mujibu wa watafiti Meagan Jacobs, Susan Levine, Kate Abney na Lester Davids katika kazi yao Fifty Shades of African Lightness.

Mratibu wa Usajili wa Majengo na Bidhaa za Chakula na Vipodozi wa Shirika TBS, Moses Mbambe anasema shirika lao limekuwa likitoa elimu kwa wafanyabiashara kuacha kuuza vipodozi vyenye viambata vya sumu kwani vinamadhara kwa watumiaji.

Anasema endapo wanavikuta vipodozi hivyo sokoni ambavyo vimepigwa marufuku au havijasajiliwa uwa vinakamatwa na kwenda kuharibiwa kwa mujibu wa sheria ya viwango.

“Tunapomkamata mfanyabiashara mwenye vipodozi hivyo anapata hasara mara mbili ikiwemo ya kuteketeza vipodozi vyote ambavyo vimepigwa marufuku auvile visivyosajiliwa na gharama ya uteketezaji ulipwa na mfanyabiashara huyo,”anasema

Anasema TBS inamifumo mbalimbali ambayo inatumika katika kuhakikisha vipodozi vyenye madhara havifikii jamii kwa kutumia mifumo ya usajili wa vipodozi vinavyoingia na vinavyozalishwa nchini hii inasaidia kuangalia viambato vilivyopona kuangalia kiwango.

Anasema mfumo mwingine ni wa ukaguzi kabla ya kuingia nchini kama vinakidhikiwango cha kuingia nchini, na mfumo mwingine ni ukaguzi sokoni baada ya bidhaa kuwa sokoni mara kwa mara kutokana na wafanyabiashara baadhi wanaingiza bidhaa nchini kupitia njia zisizorasmi.

“Asilimia kubwa ya watu wanaoingiza vipodozi vyenye viambata vya sumu mara nyingi hawaingizi kwa njia halali wanaingiza kwa njia zisizo za halali kama Bandari Bubu,lakini tunahakikisha sokoni tunafanya ukaguzi na kuvikamata mara kwa mara,”anasema

Anasema wananchi wanapaswa kutambua kuwa wao ni wadhibiti namba moja wa bidhaa za vipodozi na wao wanawajibu wa kulinda afya zao na kutotumia vipodozi ambavyo vinaviambata vyenye sumu ambavyo vinabadilisha rangi ya ngozi.

Aidha anasema vipodozi hivyo vinakuwa na sumu na sumu hiyo inapojikusanya muda mrefu katika mwili uleta madhara makubwa.

“Endapo wananchi wataacha kununua vipodozi hivi hakuna mfanyabiashara atakaenunua ni vema watakapokutana na vipodozi hivyo watoe taarifa kwa Ofisi yetu na sisi tutafanya kaguzi ya kuviondoa vyote,”anasema na kuongeza kuwa

“Kama wananchi hawavifahamu vipodozi hivyo wanaweza kutembelea katika tovuti yao na kujua ni vipodozi gani ambavyo vinaviambata vya sumu na kuacha kuvitumia ili kuweza kuokoa maisha yao na kuinua kipato cha familia kabla ya kupata maradhi,’’anasema

Baadhi ya vipodozi vyenye madhara vikisubiri kuharibiwa

Pia anasema wafanyabiashara nao wanawajibu wa kupeleka sokoni bidhaa ambazo zinakidhi viwango na sio zinazoweza kuleta madhara kwa watumiaji,”anasema

Anasema hadi sasa TBS imesajili bidhaa nyingi za vipodozi zaidi ya 400 katika soko katika kipindi cha miezi 12.

“Tumekuwa tukikamata sana vipodozi visivyokidhi viwango na vyenye viambata vyenye sumu,”anasema